December 30, 2019


WAKATI homa ya pambano la watani ikipanda, huko Yanga unaambiwa mabosi wa timu hiyo, wameweka tofauti zao pembeni na kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanamfunga mtani wao, Simba.

Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa timu hizo mbili kongwe, limepangwa kupigwa Januari 4, mwakani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zitakutana kila moja ikiwa na benchi jipya la ufundi, Yanga wenyewe wataongozwa na Kaimu Kocha Mkuu, Charles Mkwasa aliyechukua nafasi ya Mkongomani Mwinyi Zahera huku Simba wakiwa na Mbelgiji Sven Vanderbroeck aliyemrithi Patrick Aussems.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, mabosi hao walikuwa tayari kufungwa na timu yoyote katika ligi lakini siyo watani wao Simba.

Mtoa taarifa huyo alisema mabosi hao wameweka tofauti zao pembeni huku wale baadhi ya viongozi waliotofautiana kipindi cha uchaguzi uliomuweka madarakani mwenyekiti Dk Mshindo Msolla na wale wengine waliokuwepo nje ya timu wakiwa sawa kuhakikisha Mnyama anakufa Taifa, Jumamosi ijayo.

Mtoa taarifa huyo aliwataja baadhi ya viongozi hao ni Hussein Ndama, Hussein Nyika, Seif Magari, Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Samuel Lukumay na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde ambao wamejipanga kuhakikisha wanawafunga watani wao.

Aidha, aliongeza kuwa katika kuhakikisha wanaondoa hofu ya hujuma, viongozi wamepanga kuwalisha yamini wachezaji wake wote kambini mara baada ya mchezo wao dhidi ya Biashara ambao utapigwa Uwanja wa Uhuru keshokutwa Jumatatu.

“Kama unavyojua hivi karibuni uongozi mpya ulitofautiana na baadhi ya wale wa zamani katika masuala mbalimbali likiwemo suala la mauzo ya jezi mpya kabla ya GSM kushinda zabuni ya kuuza jezi.

“Hizo tofauti zao wameziweka kando kwa hivi sasa wakati wakielekea kwenye pambano la watani wa jadi na hiyo ni kawaida kutokea wakati tukielekea kwenye mchezo huo wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga, hivyo usishangae.

“Katika hizi timu kutofautiana kawaida sana, lakini linapokuja suala la pambano la watani wa jadi, basi watu wanaungana kwa pamoja ili kuhakikisha kila mmoja anapata ushindi.

“Lakini kwa Yanga wenyewe wameonekana kuungana wote kwa pamoja ili wapate ushindi na viongozi wao wamepanga kuwatumia wazee wao katika kuwalisha yamini wachezaji wake wote mara baada ya kuingia kambini kujiandaa na pambano hilo kwa hofu ya kusalitiwa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumzia hilo, Ofisa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa: “Mechi ya watani wa jadi siku zote zinawakutanisha watu kwa kuungana kwa pamoja ili kuhakikisha wanapata ushindi.

“Lakini nisingependa kulizungumzia hilo suala wakati tayari tuna mchezo mmoja kabla ya kukutana na Simba, hivyo akili zetu tumezielekea mchezo na Biashara United na Tanzania Prisons."

3 COMMENTS:

  1. Kumbe viongozi wa Yanga bado wana tafauti baina Yao. Hali hiyo ndio itayomfagilia Mnyama ambapo kwao ni shuari na kumenona

    ReplyDelete
  2. kweli simba ni chiboko,wachezaji wamelipwa wote mabosi tofauti pembeni ole wenu mfungwe timbwili la asha ngedere cha mtoto

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic