December 30, 2019


KOCHA wa timu ya Yanga, Charles Mkwasa amesema ushindi walioupata kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons umewapa nguvu ya kujipanga kuikabili Biashara United katika mchezo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Mkwasa alitoa kauli hiyo juzi baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi kwa kuifunga Tanzania Prisons bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora Iringa, na kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 21.

Alisema wanauchukulia mchezo huo kama fainali kwa kuwa ni moja ya timu zinazoonesha ushindani mkubwa kutafuta matokeo hususani kwenye viwanja vya ugenini.

“Ninawashukuru wachezaji kwa ushindi tuliopata kwani umetuongezea nguvu ya kujipanga kwenye mchezo wetu unaokuja dhidi ya Biashara United kuhakikisha tunapata matokeo kama haya kujipanga na mchezo wetu wa Januari 4 dhidi ya Simba,” alisema Mkwasa

Alisema mchezo uliopita walicheza kwa kiwango cha juu kwa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza lakini wachezaji wake walikosa umakini na kushindwa kumalizia kupata mabao ambayo yangewafanya kumaliza mchezo kipindi cha Kwanza.

Alisema kipindi cha pili wapinzani wao walicheza mpira wa nguvu na kupiga vikumbo kuwatoa mchezoni jambo ambalo walifanikiwa lakini alitoa maelekezo kwa wachezaji wake kurudi nyuma kulinda ushindi waliopata kipindi cha kwanza.

Naye kocha wa Tanzania Prisons, Mohamed Rishaard ‘Adolf’ alikubali matokeo na kukiri kufanya makosa katika dakika za mwanzo na kufungwa bao jambo ambalo hakulitegemea.

“Sina sababu ya kusema uwanja shida lakini kimsingi tulifanya makosa na kuruhusu kufungwa bao la kizamani jambo ambalo sikutegemea, nimekubali kama benchi la ufundi tunaenda kujipanga na ratiba ya mechi zinazokuja kuhakikisha tunapata ushindi” alisema Adolf Alisema matokeo hayo kwa kiasi fulani yamevuruga malengo yao kwani ilikuwa ni kulinda rekodi yao ya bila kufungwa lakini kukosa umakini dakika za mwanzo zimewafanya wafungwe.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic