December 16, 2019



NA SALEH ALLY
SUALA la uvumilivu kidogo limekuwa na ugumu sana katika mpira wa Tanzania. Huenda katika nchi nyingine kunaweza kuwa na afadhali kidogo.


Mashabiki wa soka nchini, wanataka matokeo ya papo kwa papo kwa kila kitu. Kweli hili jambo linawezekana lakini hutegemea kipi kimetokea.

Hapa ninataka kumzungumzia Kocha Mkuu mpya wa Simba, Sven Vanderbroeck ambaye anaonekana kuwa ametua na kuonekana ni matumaini makubwa kwa kikosi cha Simba kurejea katika kile ambacho mashabiki wanakitaka.

Kocha aliyeondoka, Patrick Aussems, pia ni raia wa Ubelgiji kama kocha huyu mpya, hakuwa amefeli katika kiwango cha kuonekana hawezi lakini uongozi kupitia vipimo vyao, huenda wamechungulia mbele na kuona kuna jambo linafuatia juu yao, si sahihi.

Hivyo wameamua kumuondoa na kuleta kocha mpya. Maana yake kwa mashabiki ikiwezekana hata viongozi watataka kuona mabadiliko ya haraka kwa kuwa wanaamini wana timu nzuri.

Hali hii ya uharaka, husababisha papara na jambo hili wakati mwingine pia husababisha mvurugano na tafrani inayoweza
kusababisha hata chombo kuyumba.

Ndio maana nikaamua kuwakumbusha kwamba katika soka vitu ni hatua. Kwamba unaanza na hiki, kinaingia kile hadi kufikia malengo, mfano wa kujenga kitu bora na imara. Kukiwa na haraka, kunaweza kusababisha kupita njia ya mkato na matokeo yakawa si yale yanayotarajiwa.

Niwakumbushe, kocha huyo hawezi kufanya miujiza, yeye si malaika.

Inawezekana kabisa, Vanderbroeck akaanza
kwa kasi ya ndege za kijeshi, lakini bado anaweza kuanza kwa mwendo wa treni kabla ya kuchanganya baadaye na kuwa bora zaidi.


Nasema hivyo kwa kuwa ameichukua timu ikiwa kwenye ligi tayari, bahati nzuri aliyopata kulikuwa na muda kidogo wa maandalizi. Ana nafasi ya kwenda na kikosi chake lakini hawezi kufanya mabadiliko makubwa maana anaweza “kutingisha” mfumo mzima wa kikosi.


Kwa kuwa hatabadili vitu vingi kwa wakati mmoja, lazima atakwenda na mwendo wa Aussems kwa muda fulani akienda anaupunguza taratibu hadi utakapoondoka kabisa. Huu ndio mfumo mzuri wa kocha mpya kuingiza mfumo wake ndani ya kikosi.


Sasa wakati anaanza kuyafanya hayo, kusiwe na papara na lawama, mshangao na malalamiko mapema sana hasa kwa wale ambao huenda pia hawakufurahishwa na kuondoka kwa Aussems ambaye bila ubishi kwa alichokifanya Simba kwa wakati wake ni kikubwa na kinastahili heshima.


Kocha yeyote akiungwa mkono na kama kweli ana uwezo, basi atafanya vizuri na hasa mwanzoni kwenda mbele. Ingawa mara nyingi zaidi, mwanzo kunaweza kukawa na utaratibu niliouelezea.


Ili afanye vizuri zaidi, mashabiki wa Simba wanapaswa kujikaza na kumsahau Aussems,
halafu waangalie kazi ya Vanderbroeck
inaendaje. Wakisifia au kukosoa iwe kupitia kazi yake bila ya kulinganisha kwanza.
Baada ya muda, wanaweza kuwa huru kufanya wafanyavyo. Lengo ni kumsaidia aende vizuri wakati anaanza.

Kama hakutakuwa na uvumilivu kwa kiwango fulani. Basi kuna uwezekano mkubwa wa kila kocha kuonekana hafai kila
baada ya muda mfupi.

Angalia, aliyoyafanya Aussems ni historia kwa Simba na yametokea si baada ya muda mrefu sana yeye kuwa katika usukani wa kocha mkuu. Leo naye ameonekana hana nguvu ya kuendeleza kutoka hapo. Huu unaweza kuwa uthibitisho wa uvumilifu wa mwanzoni na kuunga mkono jitihada za kocha mpya, zina manufaa.


Kocha mpya mara nyingi anakuwa na vitu vinavyoweza kushangaza, kuudhi au kukasirisha kwa kuwa vinakuwa si vya kutarajiwa.


Mfano, anaweza kumchukua mchezaji kama Shomari Kapombe akasema anataka acheze namba kumi kutokana na mtazamo wake na
alichokiona. Hii inabidi isionekane kama jambo baya badala yake kusubiri na kujifunza ili kuona itakuwaje.


Mchezaji Abdi Banda alitokea Coastal Union akiwa beki wa kushoto. Alipotua Simba baada ya muda akabadilishwa na kuwa beki wa kati. Wengi wakalalamika na baadaye akaanza kuonekana anafaa zaidi katika namba hiyo. Leo unaona yuko Afrika Kusini akiitumikia Highlands Park akitegemewa kama beki wa kati.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic