December 22, 2019


Kwa wanaokumbuka enzi za utawala wa kocha Sir Alex Ferguson ndani ya Manchester United, licha ya kuwa alikuwa anapenda watu wapambanaji wanaoweza kujituma, lakini ilifikia hatua akamuua kumruhusu nahodha wake hodari, Roy Keane aondoke.

Hivyo ndivyo ambavyo kocha wa sasa wa timu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer anatakiwa kuchukua maamuzi magumu ya kumruhusu staa wa timu hiyo, Paul Pogba kuondoka.

Pogba hajaichezea United tangu Septemba mwaka huu, amekosa michezo mingi na ameshi-ndwa kuwa na msaada mkubwa kwa timu yake kwa wakati wote huo.

Kinachotokea sasa kinaweza kufananishwa na kilichowahi kumtokea Keane enzi za utawala wa Fergie kwa kuwa nguvu ya mchezaji huyo ilitaka kuwa kubwa kupitiliza na ndiyo maana mwaka 2005 akaambiwa ‘chimba’ baada ya kutaka kumpanda kichwani bosi wake.

Keane alitoa kauli zilizokuwa zikiwaponda wenzake kupitia mahojiano yake na kituo cha runinga kinachomilikiwa na Manchester United (MUTV).

Aliwaponda Darren Fletcher, Rio Ferdinand na John O’Shea ambao kipindi hicho walikuwa wakichipukia.

Japokuwa mahojiano hayo hayakuwahi kurushwa hewani lakini ilionekana ni kama dalili za kuwakatisha tamaa vijana wadogo, wakati sera ya Ferguson ilikuwa ni kuwa na wachezaji walio tayari kupigana ‘vita’ kwa ajili ya timu hiyo.

Pogba naye alilalamika kiasi fulani kuhusu maandalizi ya timu hiyo kabla ya msimu kuanza hasa kwenye suala la baadhi ya miundombinu.

Hilo likapita kimyakimya, wakati huohuo, wenzake walianza mazoezi ya kujiandaa na msimu huu wa 2019/20, yeye akiwa kwenye mapumziko maalum baada ya kuitumikia timu ya Taifa ya Ufaransa.

Tetesi za kuwa anatakiwa na timu kadhaa za Ulaya ni kama zimeendelea kumvuruga kwa kuwa hata kauli za Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane kuwa anamhitaji nazo ni kama zimeendelea kumfanya atoke nje ya mstari.

Huu sasa ni mwezi wa tatu hajaitumikia timu yake kutokana na kuwa majeruhi, wakati huu Solskjaer kichwa kinamuuma kwa kuwa ratiba ni ngumu na mechi ni nyingi, msaada wa mtu kama Pogba ni muhimu kwake, lakini hilo limekuwa na giza.

Wakati akiwa bado anazu-mbuliwa na maje-raha, wiki kadhaa zilizopita akaonekana akiwa Marekani kwenye uwanja wa kikapu katika Ligi ya NBA.

Baadaye akajirekodi video akiwa Dubai, akiwa huko akakutana na Zidane na wakazungumza, picha zikapigwa wakiwa pamoja ufukweni.

Solskjaer akamtetea kuwa hana tatizo na wawili hao kukutana ufukweni na kuzungumza. Ni kama vile alitaka kutuliza upepo tu kwa kuwa Zidane ameshanukuliwa mara kadha akisisitiza kuhitaji huduma ya Pogba katika kikosi chake, hivyo kukutana ufukweni inaweza kuwa ni sehemu ya ushawishi kumvuta.


Hilo likapita, siku chache zilizopita, Pogba akaonekana akiwa kwenye harusi ya kaka yake, akicheza na kufurahia na familia kama vile hana tatizo la kifundo cha mguu ambalo ndilo limesa-babisha awe nje kwa muda mrefu.

Video hiyo ikasababisha gumzo kuibuka mtandaoni, baadhi ya mashabiki wakamshutumu kuwa anataka kuondoka ndiyo maana anafanya visa tu.

Kauli za kushutumiwa kwa aina hiyo ya matukio siyo mara ya kwanza, lakini mara zote Solskjaer ni kama ameendelea kuwa kimya au kutoonyesha kauli za kuwa mkali dhidi ya Mfaransa huyo.

Inavyoonekana ni kama Pogba yupo Man United kwa kuwa ana mkataba lakini hana moyo wa kuendelea kuichezea timu hiyo, kukosa moyo wa kuichezea United ni kitu ambacho Solskjaer hakitaki.

Solskjaer amekuwa na falsafa kama ilivyokuwa kwa Ferguson ya kutaka wachezaji kupambana na kujituma kwa moyo, kuacha uzembe na wale wote ambao wanaonekana hawana moyo huo huwa hawana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Thamani ya pauni 89m iliyotumika kumsajili Pogba akitokea Juventus inaonekana ni kama imekuwa kikwazo kwa United kumruhusu aondoke kwa bei rahisi.

Pogba alisababisha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Jose Mourinho kufukuzwa kazi, lakini sasa uwepo wake ni kama unaiumiza timu hiyo, inavyoonekana haijapata ofa sahihi au inambakiza kwa sababu za kibiashara.

Wakati ikitegemewa kuwa angerejea katika mchezo wa juzi, ikatangazwa kuwa hatakuwepo, kuhusu hilo, Solskjaer akasema: “Afya yake haipo vizuri, anaumwa, hakuwa na muda wa mazoezi kwa siku mbili tatu hivi, hilo limemrudisha nyuma kidogo katika kurejea uwanjani.”

Wikiendi hii, Man United inatarajiwa kukipiga dhidi ya Watford, mashabiki wa United wanasubiri kuona kama atakuwa fiti kuweza kucheza baada ya kukosa mechi 21 msimu huu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic