USHINDI ambao wameupata wachezaji wetu wa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17 mbele ya Burundi ni zawadi kwa mashabiki na mwanzo mzuri kwa timu yetu ya Taifa ndani ya mwaka 2020 hawajatupotezea muda wetu uwanjani.
Mengi yatasemwa juu yao ila wasifikiri kwamba wamemaliza kazi hapana bado wana safari ndefu kwenye kufikia mafanikio ambayo wanayafikiria kwa sasa na yale ambayo yapo kwenye mawazo ya mashabiki wengi wa soka.
Bakari Shime ambaye ni kiongozi mkuu kwenye benchi la ufundi akiwa pamoja na Edna Lema wameanza vizuri na wanastahili pongezi kwa ushindi wa mabao 5-1 katika hili wanastahili pongezi kwani ni mwanzo mzuri.
Ukiwa nyumbani ni faida kupata ushindi kutokana na aina ya wachezaji ambao unakuwa nao na mashabiki ambao wapo uwanjani kuipa sapoti timu yako basi wachezaji wanaona raha kufunga na kushangiliwa na matokea yake ushindi unapatikana.
Licha ya kushinda bado kuna makosa madogomadogo ambayo Shime mwenyewe amesema ameyaona katika hili sina mashaka naye atayafanyia kazi na ataushangaza ulimwengu kwenye mchezo wa marudio ni jambo la kusubiri na kuona nini kitatokea.
Ushindani kwenye kila mechi ni mkubwa na maandalizi huwa yanakuwa tofauti kulingana na aina ya mchezo ambayo unakwenda kucheza, kila la kheri kwenye maandalizi pamoja na mashabiki kuendelea kutoa sapoti kwa wachezaji wetu na timu ya Taifa kiujumla.
Uwepo wa mashabiki ni kitu kisichoepukika kwenye suala la uahindani na kupata matokeo mazuri ile amshaamsha ya mashabiki ni muhimu uwanjani na inaleta raha kwa wachezaji kusikia namna gani wanapewa sapoti.
Leo jamvini napenda kuzungumzia juu ya michuano ya kombe la Shirikisho ambalo kwa sasa lipo hatua ya 32 bora ya ushindani wake ndani ya ardhi ya Tanzania.
Kuelekea kwenye michuano hii ni vema timu zote zilizotinga hatua hii kujiandaa vema na kupambana kupata matokeo ndani ya uwanja kwani zikiwa zinakwenda na matokeo mfukoni zitaambulia maumivu.
Ushindani ukiwa mkubwa huku utakuza soka letu na kufanya bingwa atakayepatikana awe yule anayestahili na ataweza kupeperusha bendera ya taifa kwenye michuano ya kimataifa.
Naona kuna timu ambazo zimeanza kukata tamaa mapema kutokana na aina ya timu ambayo wamepangwa nayo huo woga haupaswi upewe nafasi kwenye maisha ya soka.
Maandalizi mazuri yatazifanya timu zote kupata kile ambacho wanastahili ndani ya dakika tisini hakuna timu ambayo imeandikiwa kushinda mechi zote hilo halipo.
Kila timu ina nafasi ya kushinda iwapo itajiandaa vizuri na kukubali kufanyia kazi makosa ambayo waliyafanya kwenye mechi zao ziizopita sio hizi za Shirikisho kwani kwa sasa ni mtoano.
Timu ikipoteza mchezo kwa sasa inatolewa kwenye michuano ndani ya mwaka 2020 hivyo inapaswa kuchukulia mchezo wao kuwa ni fainali. Siku zote fainali ni lazima ipate mshindi hivyo kinachotakiwa kufanyika ni maandalizi mazuri.
Wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi ni muda mwafaka wa kutazama ni wapi ambapo kuna upungufu mkubwa kisha wakaziba mapengo hayo na kuacha timu kuwa kwenye ushindani.
Imani yangu ni kwamba kila timu ikifanyia kazi makosa na kujipanga vema itaongeza ushindani ndani ya kombe la Shirikisho ambalo kwa sasa lipo mikononi mwa Azam FC.
Wahenga walisema kuwa penye nia pana njia timu ambazo zitaonyesha nia ya kulitafua kombe kwa moyo mmoja basi njia itaonekana na wataweza kulitwaa kombe.
Wengi watafikiria kuhusu kusafiri na gharama baada ya kulitwaa taji hili kwa kuwa watashiriki michuano ya kimataifa hilo lisiwape taabu kwani hata iliposhinda Mtibwa Sugar wengi walisema kwamba hawataweza kusafiri ila mwisho wa siku walikwea pipa na wakashiriki vizuri kabisa.
Ni wakati wa kila timu kuja na mkakati wao kwa sasa nao wawe wa kimataifa kwani hakuna timu ambayo inatakiwa iwe ya kimataifa bali timu zote zina nafasi ya kukwea pipa na kuleta mafanikio.
Wachezaji wanapaswa walitazame kombe hili kuwa ni la faida kwao kutokana na kazi yao kutazamwa duniani kote hasa kwa zama hizi za tekonolojia kuwa kubwa.
Pale ambapo wanacheza wasisahau kwamba kuna mawakala ambao wanawafuatilia endapo watakuwa ndani ya vigezo vyao inakuwa rahisi kwao kupewa mkataba na timu kubwa nje ya zile wanazozichezea.
Kupata kwao nafasi ya kutoka nje ya nchi hakuji kimiujiza bali ni kwa kuonyesha uwezo halisi ndani ya uwanja kupitia mashindano ambayo wanashiriki bila kujali nani anawasimamia.
Suala la kudhrau mashindano eti kisa hayatuhusu hatuwezi kupata faida linaua uwezo wa wachezaji na kuwafanya wacheze chini ya kiwango hasara inakuwa kwa timu pamoja na mchezaji kiujumla.
Kwa sasa zama za hofu muda wake umekwisha bali ni muda wa kuthubutu na kufanya kweli katika yale ambayo tunafikiria hasa kwenye ulimwengu wa soka.
Matumaini yangu waaamuzi watafuata sheria 17 za soka wakati wa kuchezesha mechi zote jambo litakalofanya kila timu kupata matokeo ambayo wanayahitaji hivyo ni wakati wa kila timu kujipanga kwa ajili ya ushindani.







0 COMMENTS:
Post a Comment