January 3, 2020


GUMZO lililopo nchini kwa sasa ni juu ya mechi ya watani Simba na Yanga. Vuguvugu la mechi hiyo liko juu kwelikweli kwa sababu kila moja inataka kupata ushindi mbele ya mwenzake.

Kesho, Januari 4, Uwanja wa Taifa kutakuwa na patashika kwa wababe hawa kupimana nguvu huku kila mmoja akipewa nafasi ya kushinda endapo atajipanga.
Mara ya mwisho walipokutana Yanga walilala kwa bao 1-0 huku shujaa wa Simba akiwa Meddie Kagere aliyefunga bao hilo pekee. Sasa safari hii Yanga ambao watakuwa ugenini watataka kulipa kisasi kwa wenzao na kuhitimisha safari ya mechi nne bila ya kushinda hata moja.
Wakati wakiwa wanataka kulipa kisasi hicho kuna watu wa Simba ambao wanatakiwa kuwaangalia kwa jicho la ukaribu kwa sababu wakiwaacha tu watawaadhibu tena. Katika makala haya kuna wachezaji ambao kwa pande zote mbili wanatakiwa kuwa nao makini sana kwa sababu wakiwaacha tu mambo yataharibika.

Meddie Kagere
Mnyarwanda huyu yuko kwenye kasi kwelikweli kwa sababu muda huu anakimbiza katika chati ya waliofunga mabao mengi. Anayo tisa huku akifuatiwa na Paul Nonga na Daruesh Saliboko wote wana mabao saba wapo Lipuli.
Bado Yanga wanamkumbuka kwani ndiye aliyepelekea ‘msiba’ msimu uliopita akifunga bao pekee la Simba na kama Yanga wasipokuwa nae makini atawaumiza tena.
Kagere amekuwa mjanja sana na si rahisi kumkaba ndiyo maana hadi sasa ana mabao tisa. Yanga wanatakiwa kumuundia kamati ya kumzuia.

David Molinga
Licha ya kufunga mabao kwa kawaida lakini amejitambulisha kama mtu wa hatari wa kufunga kwa faulo ambapo Simba wanatakiwa kuwa makini wasifanye makosa kwenye eneo la hatari.
Mkongomani huyu anapokuwa uwanjani si mtu wa kukaa eneo moja kitu ambacho kinamfanya awe ngumu kutulizwa na mabeki wengi anaokutana nao. Hadi sasa amefunga mabao manne akiwa ndiye anaongoza kwa wafungaji wenye mabao mengi katika klabu yake.

Miraji Athuman ‘Sheva’
Ameingia na zali la kipekee ndani ya Simba kwa sababu yuko nyuma ya Kagere kwa waliofunga mabao mengi klabuni kwake. Ana mabao sita na mara nyingi anatumika kama silaha ya kuja kumaliza mchezo ‘sub’.
Yanga pale ambapo watamuona Sheva akiwa uwanjani wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa sababu ni mwepesi kufunga sambamba, kutengeneza nafasi na kupiga mashuti kwa wapinzani.

Patrick Sibomana
Jamaa amekuwa mwokozi wa Yanga pale ambapo mambo yanaonekana kuwa magumu akifunga mabao muhimu yanaipa timu hiyo pointi katika mechi zake za ligi lakini hata walipokuwa kwenye michuano ya kimataifa.
Sibomana ambaye hati yake ya kusafiria inamuonyesha ni raia wa Rwanda hadi sasa ameweka kambani mabao manne huku akiwa mtu hatari katika kupiga faulo na kutengeneza nafasi kwa wenzake. Simba wanatakiwa kumuangalia sana.

Ditram Nchimbi
Ishu kubwa iliyomfanya akatua Yanga ni baada ya kuwapiga mabao matatu ‘hat trick’ ambapo kwenye mechi hii anapaswa kuchungwa kwani anajua kufunga lakini pia kukaa eneo sahihi na kuwasumbua mabeki.
Nchimbi alikaririwa kwamba katika mechi hii ataonyesha kwamba alistahili kusajiliwa Yanga au la, kwa hiyo ni wazi atakuwa amepania hivyo Simba wawe macho katika kumchunga.

Clatous Chama
Wakati fulani alionakana kama chemli iliyoisha mafuta na kuanza kusinzia kabla ya siku za karibuni kurudi katika uwezo wake ule wa msimu uliopita.
Jeshi zima la Yanga linatakiwa kuwa macho na Chama kwa sababu uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho umerejea tena na kitendo cha kumsahau tu kitawamaliza kwa kupitisha mipira kwa washambuliaji wake. Ana asisti mbili pamoja na bao moja katika ligi.

Ibrahim Ajibu
Katika mechi iliyopita walipokutana ndiye aliyevaa ‘usinga’ wa Yanga akiwa kama nahodha lakini safari hii yuko zake Simba. Yanga wanalijua balaa la jamaa huyo linapokuja suala zima la kutengeneza asisti kwani msimu uliopita alitengeneza 17.
Wanachotakiwa kukifanya Yanga ni kutomuacha hata nukta moja kiungo huyu kwani ikitokea hivyo atawaharibia siku yao. Hadi sasa ana asisti tatu katika klabu yake ya Simba.

2 COMMENTS:

  1. Hakuna lolote labda yatokee masjabu ila kwa Simba Yanga wajiandae kisaikolojia. Hakuna bolingo au sijui Nchimbi Yanga inakusanya wachezaji dakika za mwisho kuelekea mechi kubwa kama ya simba kama vile wanakwenda kucheza ndondo? Yanga watambue kuwa hii sio Simba ya Patrick Ausems kwamba ukimzibia game plan yake umeshamueza. Wanakwenda kucheza na Matola aliekuwa akiwasumbua kila walipokutana nae na timu alizokuwa akizifundisha licha yakuwa alikuwa na vikosi vya kawaida. Pale Simba Matola ni Simba na ameungana na vijana wake kadhaa aliokuwa akiwafundisha tangu wakiwa vijana wadogo kabisa mambo wanaelewa kabisa nini ya maana halisi ya mechi ya simba na Yanga kwa hivyo wacha Mungu atufikishe kwa salama kesho tuone kitakachotokea kwani hata Mazembe na Alhaly ya Egypt wameshindwa kuifunga Simba Daresalaam na Yanga wanaoiona Simba timu ya kawaida na kama kweli wataingia uwanjani na mawazo hayo basi baada ya mechi wasije wakaanza kufukuzana. Na kwa YANGA Simba wakitafuta mtu sahihi wakucheza na Yondani Yanga kwisha habari. Simba wanaweza kumtoa mchezoni Kevin Yondani dakika za mwanzo tu za mchezo.Ni mchezaji asiekuwa na nidhamu ana hasira za kijinga akikutana na fowadi msumbufu mara kadhaa amekuwa akicheza rafu za kijinga na benchi la ufundi la Simba wakitambua hilo basi Yanga inaweza kucheza timu pungufu karibu muda wote wa mchezo.

    ReplyDelete
    Replies
    1. acha unafiki.
      leo unaiona timu ya ausens si kitu,
      kwa miaka 10 ni kocha yupi kawafikisha robo final.
      tabia hizo za wanawake wasiojielewa.
      leo unamuona broek ni bora kwa mwez mmoja, kiliko usens wa mwaka mzimaaliyewatambulisha upya afrika?
      nina wasiwas huenda siku moja ukamkataa mama yako

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic