January 12, 2020


LEO Jumapili, timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 watakuwa na kibarua cha kupambana na timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17 ya Burundi.
 Timu hizo zitapambana katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam wakati timu hizo zikisaka tiketi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia, India, mwishoni mwa mwaka huu.

Utakuwa ni mchezo wa aina yake  ambao wawakilishi wa Tanzania, U 17 wanatakiwa kupambana kwa kupata ushindi wa nguvu wakiwa hapa nyumbani.

Kupata matokeo makubwa hapa nyumbani kutaipa Tanzania nafasi kubwa zaidi kuona inafanikiwa kucheza michuano hiyo mikubwa.

U 17 wakicheza leo, wataelekea Burundi kwa ajili ya mchezo wa marudiano unatarajiwa kupigwa mapema Januari 25, mwaka huu nchini Burundi na kama watafanikiwa kuitoa  basi Tanzania wao watacheza na Uganda katika hatua inayofuta.

Lakini ushindi ambao wamejipanga kupata U 17 hauwezi kuja hivihivi bila sapoti kutoka kwa watanzania  hivyo ni vizuri tukajitokeza kwa kwenda kuisapoti timu yetu.

Sapoti kubwa ambayo watapata kwa Watanzania hakika itakuwa ni furaha kwetu na itatujenga kuona timu yetu inafika mbali zaidi ya hapa tulipo sasa.

Tunaamini ndoto ya U 17 ni kuona inafanikiwa kufuzu na kucheza Kombe la Dunia na sio wao pekee hata watanzania wanatamani kuona hilo linatokea kwa timu yao kufanikiwa kufuzu michuano hiyo.
Uwanja  wa Taifa ukijaa leo litakuwa ni jambo la kheri na la kishujaa kwa timu yetu kwani itapata nguvu zaidi  na kuongeza bidii sababu watajua kabisa kuna watu nyuma yao ambao wanawatakia wao mema katika mafanikio yao.


Ni mechi muhimu ambayo watacheza, lakini pia matokeo mazuri ni muhimu  kwenye uwanja wa nyumbani na kila kitu kinapaswa kumalizika hapa na sio kusubiri  mechi ile ya marudiano tena tukiwa ugenini.
Soka la wanawake kwa sasa linakuwa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa uwingi na kujiunga na timu hizo na tunaamini  miaka ijayo Tanzania itakuwa na timu bora za wanawake kutokana na vyombo husika vinavyopambana kuhakikisha wanasapoti soka hilo ambalo nyuma halikupewa kipau mbele kabisa.

Hivyo ni vyema kuwaunga mkono wanawake kwa kwenda uwanjani kuwasapoti kwa nguvu zote hakuna kinachoshindikana, tunaamini kuwa wanawake wanaweza.
 Kila la kheri U 17 piga hao Burundi ndoto ya kucheza Kombe la Dunia iweze kutimia hakuna kinachoshindikana zaidi watanzania leo Jumapili tukutane taifa kwa wingi kuisapoti timu hii.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic