LEO Jumatatu, Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar kutakuwa na kazi moja tu kwa mashabiki wa mpira kushangilia timu zao za Simba na Mtibwa Sugar, ambazo zitakuwa vitani kutafuta taji la Mapinduzi Cup.
Mapinduzi Cup ilianza kuwasha moto Januari 6, 2020 ambapo jumla ya timu nane zilishiriki kwenye kombe hili ambalo mabingwa watetezi walikuwa ni Azam FC.
Hakukuwa na timu alikwa kutoka nchi jirani kama ilivyokuwa zamani ambapo timu kama KCCA na URA zimewahi kualikwa na kutwaa ubingwa wa Mapinduzi.
Timu nne kutoka Bara zilikuwa ni pamoja na Azam FC, Mtibwa Sugar, Yanga na Simba huku wenyeji wakiwakilishwa na Zimamoto, Jamhuri, Mlandege na Chipukizi.
Matukio ambayo yalibamba kabla ya kushuhudia mchezo wa fainali ya leo.
Timu za Zanzibar kutolewa mapema
Wenyeji Zanzibar walishindwa kufurukuta na kutinga hatua ya nusu fainali ambapo timu zote nne zilipigwa chini hatua ya awali na kuwaacha wenyeji watawale wenyewe kwenye ushindani.
Mlandege ilifungashiwa virago na Azam FC kwa kufungwa bao 1-0 lililopachikwa na Obrey Chirwa, Zimamoto ikafungwa na Simba kwa mabao 3-1 wafungaji wakiwa ni John Bocco, Sharaf Shiboub na Ibrahim Ajibu huku lile la kufutia machozi likifungwa na Ahmad Hilika.
Kwa upande wa Chipukizi wao walifungashiwa virago na Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya dakika 90 kukamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1 huku Jamhuri wakitolewa na Yanga kwa mabao 2-0 yalijazwa kimiani na Adeyum Suleiman na Mohamed Issa ‘Mo Banka’.
Azam FC ilitolewa na Simba kwa penalti 3-2 baada ya dakika tisini kutoshana nguvu kwa sare ya bila kufungana.
Nusu fainali
Hatua ya nusu fainali, Mtibwa Sugar ilikuwa ya kwanza kukata tiketi ya kusonga mbele baada ya kushinda kwa penalti 4-2 mbele ya Yanga ambayo ndani ya dakika 90 ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lilisawazishwa dakika za nyongeza na Shomari Kibwana wa Mtibwa Sugar.
Mabao ya nje ya 18
Licha ya kutolewa Yanga imeweka rekodi ya kufunga mabao ya nje ya 18 mengi kuliko timu zote ikiwa imefunga mabao mawili.
Adeyum Suleiman alikuwa wa kwanza kwenye mchezo wa robo fainali mbele ya Jamhuri kwa mpira wa adhabu uliozama nyavuni na bao la pili likifungwa na Kaseke aliyemalizia pasi ya Mapinduzi Balama akiwa nje ya 18 mbele ya Mtibwa Sugar.
Utamu wa fainali
Utamu wa fainali leo utanoga kutokana na timu zote mbili kutinga hatua hii kwa njia inayofanana kwa kupenya kwa hatua ya mikwaju ya penalti kwenye hatua ya nusu fainali.
Ilianza Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa inawatazama namna Azam walivyokuwa wanamenyana na Simba kwa kuifunga Yanga kwa penalti 4-2 baada ya sare ya kufungana bao 1-1. Mtibwa pia hata kwenye hatua ya robo fainali walipenya kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoshana nguvu na Chipukizi dakika 90 walifungana bao 1-1 na kushinda kwa penalti 4-1.
Simba pia imetinga hatua ya fainali kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya dakika 90 kutoshana nguvu na Azam FC ila hawa hatua ya nusu fainali walishinda mabao 3-1 mbele ya Zimamoto FC.
Wachezaji wa kuchungwa
Kwa sasa wachezaji wote wa Simba na Mtibwa ni wakali ila kwa upande wa washambuliaji, Meddie Kagere licha ya kukosa nafasi nyingi za wazi bado ana urafiki na nyavu, John Bocco mwenye bao moja sio mtu mwepesi akiwa ndani ya 18 pamoja na Ibrahim Ajibu ambaye taratibu anaingia kwenye mfumo.
Kwa upande wa Mtibwa Sugar, Jaffary Kibaya ni mbaya muda wote, Haruna Chanongo na Riphat Khamis hawa wana uwezo wa kubadili matokeo muda wowote pamoja na Kibwana Shomary ambaye alifunga bao la usiku mbele ya Yanga.
Hesabu za makocha
Sven Vanderbroeck, Kocha Mkuu wa Simba alisema kuwa yupo tayari kwa ajili ya kushinda na atafurahi kubeba taji lake la kwanza akiwa na Simba.
Zuberi Katwila, Kocha Mkuu wa Mtibwa Suagr alisema kuwa ana imani utakuwa mchezo mgumu ila wapo tayari kulitwaa Kombe la Mapinduzi bila mashaka yoyote.
Azam FC ambao walikuwa ni mabingwa watetezi watabaki kutazama fainali hiyo kwenye runinga ama kubaki visiwani huko baada ya kuvuliwa ubingwa na Simba waliowafunga mwaka jana (2019) mabao 2-1.
0 COMMENTS:
Post a Comment