January 13, 2020

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka huu wa 2020 tamati yake itakuwa leo Jumatatu ambapo itacheza mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Amaan uliopo Unguja, Zanzibar.
Kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya nusu fainali iliyochezwa kati ya Yanga na Mtibwa Sugar tulishuhudia Mtibwa Sugar ikiibuka na ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Yanga baada ya dakika tisini kumalizika kwa bao 1-1.
Yanga walikuwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo, walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa bao 1-0. Kipindi cha pili wakarudi kulilinda bao lao, wakafanikiwa hadi kufikia dakika 90.
Walifanya kosa kubwa sana katika zile dakika tatu za nyongeza kabla ya kumalizika kwa mchezo huo. Wakaruhusu Mtibwa wasawazishe bao hilo na mchezo kuwa 1-1. Wakaenda kwenye penalti.
Kama ujuavyo, watu wanasema penalti hazina mwenyewe, ndiyo ikatokea yaliyotokea, Yanga imetupwa nje ya michuano hiyo.
Tena cha zaidi ni kwamba, timu imefungwa mbele ya kocha mpya, Luc Eymael raia wa Ubelgiji ambaye ndiyo kwanza alikuwa amefika Tanzania, moja kwa moja akaenda kuishuhudia timu yake mpya ikicheza.
Kufanya kosa si kosa, bali kurudia kosa ndiyo kosa, Yanga wamerudi, sasa ni muda wa kujiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu Bara. Bado wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanatoka nafasi waliyopo na kupanda juu zaidi.
Wakati mechi ya Mtibwa na Yanga ikimalizika, Ijumaa 10, Januari ilichezwa mechi ya nusu fainali ya pili kati ya Simba na Azam. Mshindi wa mchezo huo Simba ameungana  na Mtibwa katika fainali.
Kikubwa ninachotaka kusema leo ni kwamba, michuano hii imekuwa ikifanyika kila mwaka kuelekea maazimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini wenyeji wamekuwa wakifanya vibaya.
Ukiangalia kwa mwaka huu, timu nne za Zanzibar zilizoshiriki, zote zimeishia hatua ya kwanza baada ya kufungwa.
Mwaka huu ni tofauti na miaka mingine, safari hii mechi moja tu ukifungwa unatoka, ndicho kilichotokea hatua ya awali.
Kuna cha kujifunza kwa wenyeji wa michuano hii kuangalia wapi wanakosea, kwa nini kila mwaka wamekuwa wasindikizaji tu.
Tunataka kuona mabadiliko, wakati mwingine muingie fainali mcheze wenyewe au na timu kutoka Bara au yoyote itakayoalikwa.

Katika rekodi za michuano hiyo tangu kuanza kwake mwaka 2004, JKU pekee kutoka Zanzibar ndiyo iliyowahi kuwa bingwa. Ilikuwa mwaka 2005. Baada ya hapo, hakuna timu ya Zanzibar iliyotwaa ubingwa zaidi ya Tanzania Bara na mbili zilizoalikwa kutoka Uganda. KCCA na URA.

Mwisho kabisa niwapongeze Watanzania kwa  kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kwanza wa kufuzu Kombe la Dunia 2020 kwa vijana chini ya miaka 17 upande wa soka la wanawake.

Jana Jumapili, timu yetu ya Tanzania ya wanawake chini ya miaka 17, ilicheza na Burundi mechi hiyo ya kufuzu Kombe la Dunia kwa wanawake wa umri huo ilikuwa ni ya kukata na shoka.

Ni mchezo muhimu, kupata ushindi wa mabao 5-1 si haba kwani inaonyesha ni namna gani wachezaji walijituma na kupata matokeo.

Ni wakati wa kuendelea kuwapa sapoti wanawake na kujitokeza kwa wingi uwanjani kwani kila siku kuna vitu vya kujifunza uwanjani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic