January 3, 2020


Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema mabadiliko aliyokuwa anafanya kupanga kikosi kipya kila mchezo, alikuwa anatunza nguvu kwa wachezaji wake kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga, unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi dhidi ya time yake na Ndanda FC, kocha huyo alisema kumpumzisha Meddie Kagere, Pascal Wawa na Clatous Chama ni kuwapa muda kwa ajili ya kujipanga na mchezo ujao.

“Tuna mchezo mgumu dhidi ya Yanga na tunahitaji ushindi, hivyo niliwapumzisha Meddie Kagere, Pascal Wawa na Clatous Chama ili wajipange kwa mchezo ujao,” alisema Sven.

Kocha huyo amefurahishwa na ujio wa beki kiraka Erasto Nyoni na nahodha John Bocco na kuonesha kiwango bora kwenye mchezo huo, akiamini siku zijazo atakuwa na kikosi bora zaidi cha ushindani.

Aidha, aliwapongeza wachezaji, Deo Kanda na Francis Kahata, kwa kufunga mabao yaliyoifanya timu hiyo kuibuka na ushindi na kuzidi kuwaweka kileleni mwa msimamo wa ligi na katika mbio za kutetea ubingwa.

Alisema kwenye mchezo dhidi ya Ndanda FC walicheza mpira wa kufunguka zaidi, lakini wapinzani wao waligundua mbinu hiyo na kushindwa kufuata mfumo wao hivyo kucheza taratibu kupoozesha kasi yao.

“Baada ya kutokea hali hiyo, nilifanya mabadiliko kwa kumwingiza Deo Kanda na Chama walioongeza nguvu na kupata bao la pili,” alisema Sven.

Naye kocha wa Ndanda FC, Abdul Mingange, alikubali matokeo na kusema muda mwingi walikuwa wanapoozesha mchezo na kucheza kwa kujilinda ili kupunguza idadi ya mabao.

“Tuliingia na mbinu ya kujilinda kupunguza idadi ya mabao na kweli tulifanikiwa lakini tungesema tufunguke wangetufunga mabao mengi kwa kuwa wapinzani wetu wana kikosi bora, “ alisema Mingange.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 34 na Ndanda ina pointi nane ikiwa katika nafasi ya 18 ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

2 COMMENTS:

  1. Tazama jinsi jicho la kocha huyu linavoona mbali. Ina mana mechi zake zote Alizocheza na kuhsinda zote Bila ya kupokea hata bao moja la wapinzani manaake ameshinda kwa vikosi vya kujaribu wachezaji tu na sio kikosi cha Kwanza kinyume na wale wapiga majisifu mengi. Mambo mazito na yanatia kiwewe.

    ReplyDelete
  2. Na juu ya hayo yote Mnyama Katika mchezo huo kinyume na watani, Sven hajamtumia na hatomtumia hata mchezaji mmoja wa usajili mpya. Hana papara wala majigambo anaendeshwa na bongo lake linaloona mbali.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic