Jumamosi iliyopita viungo wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na Mapinduzi Balama, walionekana lulu na wafalme, baada ya kutunzwa fedha huku wakibebwa juujuu na mashabiki wa timu hiyo.
Tukio hilo la aina yake lilitokea mara baada ya mchezo huo kumalizika wakiwa wanatoka vyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakielekea katika basi la timu hiyo.
Wakiwa wanalikaribia basi hilo, kundi kubwa la mashabiki waliwafuata wachezaji hao na wa kwanza alikuwa ni Niyonzima ambaye aliimudu vema safu ya kiungo akipambana na Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Francis Kahata na Clatous Chama.
Kundi hilo la mashabiki walimfuata kwa kuanza kumpokea mlangoni alipokuwa akitoka vyumbani hapo kwa kumbeba kisha kumtunza fedha kama sehemu ya kumpongeza kiungo huyo.
Mara baada ya kutunzwa fedha hizo, Niyonzima alionekana kuwashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kumsapoti na kumpokea tena kwa mara ya pili alipojiunga na timu hiyo katika dirisha dogo.
“Nawashukuru mashabiki wa Yanga kwa kunipokea tena kwa mara ya pili, pia nashukuru kwa kurudi salama kwenye timu yangu iliyonilea na kunipa mafanikio makubwa, kiukweli ni jambo la kushukuru unapoondoka sehemu na kurudi salama, naahidi kuwapa ushirikiano mkubwa mashabiki,” alisikika Niyonzima.
Balama naye alifuatwa na kubebwa na kutunzwa fedha na mashabiki kutokana na bao lake la ufundi la shuti la umbali wa mita 18 alilolipiga lililozaa bao la kwanza kabla Issa Mohamed ‘Banka’ kufunga la pili na kufanya matokeo kuwa sare ya 2-2.
0 COMMENTS:
Post a Comment