NA SALEH ALLY
MHIMILI wa mwendo wa Yanga kwa kipindi hiki ni wadhamini wao, ukianzia na Sportpesa ambao ni wadhamini wakuu halafu GSM, kampuni inayouza nguo, samani na vifaa vingine vya ndani kama magodoro na kadhalika.
GSM pamoja na kuwa wadhamini, imekuwa tofauti kidogo kwa kuwa wamekuwa kama ndugu wa Yanga au rafiki wa karibu ambaye yu tayari kushiriki katika matatizo ya ndugu ya rafiki yake.
Tumeona namna ambavyo GSM wamekuwa wakishiriki katika masuala ya usajili katika kikosi cha Yanga na sote tunajua, kama si wao, kungekuwa na shida kubwa kwa Yanga.
Tunajua bado Yanga hawajakaa vizuri kifedha, tunajua bado hawajawa na watu sahihi wa kukimbia huku na kule kuhakikisha mambo yanakaa sawa kwa wakati.
Pia tunajua kuwa ndani ya Yanga kumekuwa na mambo kadhaa ya kutoelewana baina ya uongozi wa sasa na baadhi ya wale waliopita ambao huenda wasingefurahi kuona hawa wa sasa wakifanikiwa, jambo ambalo sasa limekuwa la kawaida katika hizi klabu zetu na imekuwa ni sumu ya muda mrefu.
Binafsi naamini itakuwa vigumu sana kwa GSM kuwakopesha Yanga kwa kila wanachowafanyia. Pia itakuwa vigumu sawa na kwa Yanga kulipa kila wanachofanyiwa na GSM kwa maana ya kuwapa fedha. Lazima kuna sehemu nyingi mambo yanafanyika kirafiki au kimapenzi.
GSM wanataka kukuza biashara zao ambalo ni jambo sahihi kwa mfanyabiashara. Kwa mkataba walioingia na Yanga, wangeweza kukaa pembeni na kuacha mambo yaende tu kimyakimya kwa kuwa tayari wameingia mkataba na wanatoa fedha zao. Lakini tumeona imekuwa tofauti na wao wanafanya zaidi ya kile ambacho kinatarajiwa.
Injinia Hersi Said, huyu ni mmoja wa Wakurugenzi wa GSM, tumeona namna anavyopambana na kazi za Yanga. Tunakubaliana haiwezi kuwa sehemu ya mkataba, badala yake kuna ziada ambayo itaongozwa na urafiki au mapenzi ya dhati kwa kuwa kusafiri huku na kule nako ni kugumu, gharama na kunachosha lakini tunamuona Injinia Hersi amekuwa akiendelea tu.
Hapo ndipo nilipoanza kujiuliza, kwamba kwa juhudi hizi za GSM, Yanga au Wanayanga kwa jumla nao wanafanya kipi hasa kuhakikisha rafiki zao nao wanajiona kuna wanaowajali.
Mnajua, unapokuwa na urafiki na mtu Waingereza wanasema “Give and take”, kila mtu apate, maana upate kitu kizuri kutoka kwa rafiki yako.
Yanga wanatakiwa kuwaonyesha GSM wamewaelewa kuwa wao ni rafiki zao wa kweli na urafiki wao ni ule wa “Give and take”. Si wao Yanga ndiyo wawe wana “take” huku GSM wabaki hawapati kitu, nao ni wanadamu na ndiyo wanaojenga kampuni, kuna siku watachoka.
Kuwaonyesha GSM Yanga ni sehemu sahihi, au mikono ya kirafiki, wawaunge mkono nao kwa nguvu kwa kununua bidhaa zao, kuzitangaza kwa maana ya kuzithamini, jambo ambalo litawaongeza GSM morali wakiamini walio nao ni rafiki wa kweli.
Kwa GSM kujua Yanga ni rafiki zao ni rahisi sana kwao. Wataangalia hesabu za bidhaa zao katika maduka yao. Kama zitakuwa zinapanda, basi watajua Yanga ndiyo wanaofanya hivyo hata kama kuna wateja wengine.
Yanga wanunue bidhaa zao kuwaonyesha kuwa wao wapo, hata kama kuna wateja wengine nao ni sehemu kubwa ya kuhakikisha wanaendelea kufanya biashara na kuisaidia Yanga.
Kutangaza biashara maana yake ili afanye biashara yake kwa uzuri zaidi. Yanga wana wingi wa watu ambao ni mtaji mkubwa na hakuna ubishi pamoja na mapenzi hata GSM wamevutiwa na hilo.
Hivyo, Yanga wawaonyeshe basi kuwa hawakukosea na nguvu ya watu wanayo kweli na tukubaliane, kwa Yanga kuna madaraja yote ya maisha, juu, kati na chini na hii ni kutokana na idadi kubwa waliyonayo.
Hivyo, wawaunge mkono GSM ili waendelee kubaki lakini wale ambao hawajaingia kudhamini mpira au kudhamini Yanga waone watu wa Yanga au wa mpira wanaelewa thamani ya wadhamini au wale wanaojitolea katika mpira ili nao waingie na kuunga mkono mpira.
Yanga inapokuwa na nguvu, mpira wa Tanzania unakuwa na nguvu na timu nyingine nayo ikipata wadhamini, basi mambo yanazidi kuwa mazuri katika mpira na faida inashuka kupitia klabu, wachezaji na mashabiki wenyewe.
GSM imemalizika chaji na ndio mana wanaishukuru Mtibwa kwa kuwanusuru na aibu
ReplyDelete