KUTOKANA na kiwango kikubwa ambacho amekionyesha kiungo mkabaji na nahodha Mkongomani Papy Tshishimbi, Kocha Mkuu wa Yanga Mbelgiji Luc Eymael amemhakikishia nafasi ya kudumu nyota huyo.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu kocha huyo amuweke benchi Tshishimbi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara walipocheza na Mbeya City huku Said Makapu akianzishwa kabla ya kutolewa katika kipindi cha pili baada ya kucheza chini ya kiwango.
Katika mchezo huo, kabla ya Tshishimbi kuingia timu ilionekana kushindwa kuanzisha mashambulizi kutokea chini namba sita nafasi aliyokuwa anacheza Makapu kabla ya kutolewa na kuingia Mkongomani huyo kubadili mchezo na kusawazisha bao kupitia kwa Bernard Morrison aliyefunga bao kwa kichwa akiunganisha krosi ya Juma Abdul.
Tshishimbi ameonekana kuwa mhimili katika safu ya kiungo ya timu hiyo akicheza sambamba na Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Mapinduzi Balama katika michezo iliyopita.
Luc alijaribu kumchezesha namba sita Makapu kwa makusudi na kikubwa kuona uwezo wake wa kucheza nafasi hiyo kabla ya kipindi cha pili kumtoa kumuingiza Tshishimbi ambaye alionekana kubadilisha mchezo na kusawazisha bao.
Luc alikiri kukosekana kwa Tshishimbi katika kipindi cha kwanza walipocheza na Mbeya City, kulisababisha Yanga isiwe na ubora katika eneo la katikati kiungo iliyokuwa ikichezwa na Makapu na Niyonzima kabla kufanya mabadiliko.
“Nikiri kuwa Tshishimbi ni muhimu katika timu hasa kwenye nafasi yake ya kiungo namba sita, hilo amelithibitisha katika mchezo wetu uliopita wa ligi tulipocheza na Mbeya City.
“Nilifanya makusudi kumuangalia Makapu akicheza katika nafasi hiyo, pia nilihitaji kuwapa mapumziko baadhi ya wachezaji hasa Tshishimbi na Niyonzima. Hata hivyo, tumeona timu iliikosa muunganiko kukosekana kwa Tshishimbi,” alisema Luc.
Makapu alicheza vizuri kwenye mechi ambazo alitumiwa kama mlinzi wa kati namba nne akicheza pamoja na Mghana Lamine Moro kabla ya Yondani kurejesha kwenye kikosi cha kwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment