Na Saleh Ally
HAKUNA anayelalamika kuhusiana na kiwango cha mshambuliaji Ibrahim Ajibu Migomba kupitia kipaji, badala yake ni neno moja na tunapaswa kujifunza kupitia kwake.
Inawezekana watakaotakiwa kujifunza zaidi ni wale wanaochipukia, wale wanaomuamini na ikiwezekana wale wanaotamani kuwa kama yeye.
Kwa wale ambao wanapenda kuendelea na kufikia matamanio yao kisoka, pia wanaweza kumtumia Ajibu kama somo kuu la kubadili maisha yao kwa kuwa kwa miaka michache tokea ameanza kuwa maarufu, ana kitabu chenye kurasa nyingi za mafunzo.
Kocha Mkuu wa Simba, Sven van derbroeck raia wa Ubelgiji aliamua kumrudisha Ajibu katika kikosi chake cha pili ili apate nafasi ya kutosha ya kucheza na kuwa fiti hasa.
Sven ambaye ni kati ya makocha vijana waliowahi kuinoa Simba, amesema anaamini Ajibu ana kipaji na uwezo wake ni mzuri lakini anamtaka awe fiti ili kuendana na kasi ya kikosi chake.
Pamoja na hivyo, Sven amemsisitiza Ajibu kujituma zaidi ili kuweza kuingia katika kikosi cha kwanza. Hii si mara ya kwanza kwa Ajibu kuambiwa suala “kujituma” kwanza.
Inawezekana wamepita makocha wengi walisema hivyo lakini kama unakumbuka wakati akitokea Simba kwenda Yanga, gumzo kutoka Msimbazi lilikuwa kuwa Ajibu ana kipaji lakini mvivu wa mazoezi na hapendi kujituma.
Baada ya kutua Yanga pamoja na kwamba usajili wake ulikuwa gumzo, kilichotokea ni Kocha Mkuu, George Lwandamina wakati huo aliamua kumuweka benchi na kumpa mazoezi ya ziada.
Lwandamina maarufu kama Chicken aliamini Ajibu ana “madini” lakini utimamu wa mwili ambao hutokana na mazoezi magumu au makali na hasa mwanzoni mwa msimu, haukuwa sawa.
Baada ya mazoezi ya muda mrefu, alianza kumtumia. Hali kadhalika, alipoingia Mkongomani, Mwinyi Zahera naye akaona bado Ajibu alikuwa na upungufu wa utimamu wa mwili kwa maana ya fitness.
Kawaida utimamu wa mwili hulindwa, baada ya kuwa fiti kuna miiko yake ikiwemo kupumzika, kutofanya ngono zembe na kadhalika. Lakini kuendelea kuongeza mazoezi kulinda ulichonacho mwilini.
Unaona alipoingia Zahera naye aliona Ajibu ana kitu ambacho kitakuwa msaada katika kikosi chake lakini mwisho bado akaona upungufu uleule wa utimamu wa mwili.
Alichofanya ni kumuweka katika mazoezi maalum wakiwa kambini ili kuhakikisha anakuwa fiti. Wakati watu wakilalamika, Zahera hakujali akampa Ajibu mazoezi ya kutosha na alipopata nafasi katika kikosi cha kwanza akatumia ujanja kumtaka ajione ana mzigo wa kuibeba timu.
Akamvua unahodha Kelvin Yondani na kumpa Ajibu akiwa nahodha kwa mara ya kwanza katika klabu kubwa kama hiyo. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha anakuwa kiongozi.
Kama unakumbuka hili nalo lilienda kwa muda tu baada ya hapo Ajibu akaanza kukaa benchi akiwa nahodha, hali inayoonyesha alishindwa tena kutunza kiwango chake katika kiwango kinachotakiwa licha ya kwamba alikuwa ni nahodha.
Kila kocha ambaye amemfundisha Ajibu anaona jambo moja na Ajibu ameshindwa kulitatua na hili linamfanya aendelee kubaki benchi wakati akiwa na madini yake.
Kwa kifupi, madini aliyo nayo hayamsaidii Ajibu kwa kuwa anashindwa kuhakikisha anayafanyia usafi. Kuyafanyia usafi ni “simpe” tu, kufanya mazoezi ya uhakika na kuendelea kuyalinda ili aendelee kuwa fiti.
Uvivu ni adui wa maendeleo, kwa wale ambao wamekuwa wakisema ni mvivu basi inawezekana ameshindwa kumshinda adui huyo na ndio maana mwanzo nikasema wanaotaka kuwa kama Ajibu au wanaotaka kutimiza ndoto zao, wamtumie Ajibu kujifunza namna ya kupambana na adui uvivu.
Haiwezekani kasoro moja ikakushinda, ikakunyima nafasi, ikakufanya uonekane hauwezi lakini ukashindwa kupambana nayo wakati ipo ndani ya uwezo wake.
Haiwezekani una neema ya kipaji, ukakosa moyo tu wa kujituma. Ajibu si wa kukaa benchi timu yoyote hapa Tanzania na inawezekana hata angekwenda TP Mazembe alikuwa na nafasi ya uhakika ya kucheza lakini aliamua kutokwenda, huenda kwa kuwa anajitambua.
Kila mtu ana uamuzi wa maisha yake, Ajibu amechagua alivyokuwa zamani na alivyo sasa. Kitu kizuri, mtumieni kwa faida yenu na taifa kisoka, mjifunze badala ya kumshangaa, maana haiwezekani kila kocha mpya, azungumze lilelile kama la kocha aliyepita na bado ushindwe kulibadilisha.








Ukitaka kujua akiri ya Ajibu ni post yake aliyomuandikia Tshitshimbi ya fuata nyuki ule asali. Pale alionyesha kutojitambua, kwanza anaona kama kucheza Simba amemaliza safari yake hivyo kukaa benchi haimuumizi hata kidogo. Mazembe walikuwa wawazi kuuwa Ajibu hakuwa na thamani hiyo aliyojipa ila kwa sabb simba hawakuwa na uchungu na hela za Mo wakatoa tu. Unatoa milioni mia kwa ajili ya mchezaji kukaa benchi!? Mbaya zaidi umri unaenda wakati yeye anahitaji kusimamiwa muda wote!? Nafikiri kuna kitu anatumia ambacho kinamfanya asiwe sawa psychologically
ReplyDeleteNawashangaa mmewakomalia Ajib na Ndemla kama vile mnazilisha familia zao.Hawo wameshapita umri wa miaka 18 na hivyo sio watoto.Wameshapewa ushauri na wadau wa soka tena wa kupitiliza lakini imekuwa sawa na kumpigia gitaa mbuzi na wala asikusikilize na tune yako ya gitaa.Wadau wenzangu eleweni kuwa nao wana familia zao na mameneja ambao hujui wanacho washauri.Kunahitajika mahesabu ya akili kwenda kucheza soka ktk nchi za kigeni hata iwe hapo jirani zetu.Sio swala la kukurupuka na kushinikizwa.Sioni tatizo kwa uamuzi wa Ajib kwenda kucheza TP Mazembe kwani alibainisha ktk mahojiano kuwa aliangalia fungu lilowekwa mezani na akaona la Simba lilikuwa na masilahi zaidi.Unaposema angeenda tu TP Mazembe na angepigania namba kama Mbwana Samatta kwangu hiyo sikubaliani nayo sana.Ni lazima uangalie vigezo alivyoondoka navyo Mbwana Samatta na alivyo navyo Ajib kwa sasa.Mbwana aliondoka akiwa na umri wa U20 na hakuwa na familia.Ajib ni zaidi ya umri wa miaka 23 na ana familia na kama sikosei ni majeruhi kila mara.Ana kipaji na akili ya mpira lkn ukweli ni slow na simuoni kukaba na anapenda kucheza na jukwaa na ndicho MO anachompendea hivyo kwa nini asicheze kamari wakati unajua huna uhakika wa namba huko TP Mazembe maana hujui utakutana na kocha na mfumo gani wa Morinho au wa Guardialla? Mpira ni biashara na biashara ya mpira ni mahesabu hivyo tusiwe wepesi wa kuhukumu ilhali unajua wachezaji wana familia zao ambazo wanawapa ushauri pia na uamuzi wa mwisho ni wa kwake mchezaji mwenyewe atakayebeba msalaba wake huko mbele ya safari.Period!!!
ReplyDeleteBaada ya Ajibu kusaini simba aliulizwa unaonaje ushindani wa namba ndani ya simba na nafasi iko wapi? Ye alitoa jibu rahisi kuwa anafurahi amerudi nyumbani hayo mambo ya ushindani wa namba kwa huo hayajui ye anajua amerudi nyumbani!! Kwa hiyo akili ya Ajibu haipo kwenye ushindani wa namba mumuache jamani amerudi nyumbani
ReplyDelete