UONGOZI wa JKT Tanzania umesema kuwa mpango mkubwa uliopo kwa sasa ni kupata matokeo chanya kwenye mechi zake zilizobaki ili kumaliza ligi ikiwa ndani ya nafasi tano za juu.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Jamila Mutabazi amesema kuwa wachezaji wanatambua majukumu yao jambo linalowafanya waamini kwamba inawezekana.
"Kuna wachezaji wengi ambao ni wazuri ndani ya JKT Tanzania na wanatambua kwamba malengo yetu ni kumaliza ndani ya tano bora hilo lipo mikononi mwao.
"Kila kitu kinawezekana kwa kuwa tumepanga na tunatekeleza kwa vitendo ni suala la kusubiri kwani bado tuna mechi mkononi ambazo tunaamini tutapata matokeo mazuri," amesema.
Mchezo wao wa hivi karibuni Uwanja wa Sokoine walilazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na Tanzania Prisons.
Pia walipokutana na Yanga ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 mbele ya Yanga, mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri.
JKT Tanzania ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi 47 baada ya kucheza mechi 32. Imebakiwa na mechi sita mkononi.
0 COMMENTS:
Post a Comment