UONGOZI wa KMC umesema kuwa leo utapambana kusaka pointi tatu mbele ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa majira ya saa 10:00 jioni.
KMC inamenyana na Kagera Sugar leo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wake uliopita kwa kufungwa mabao 4-0 mbele ya Biashara United.
Kagera Sugar inakumbukumbu ya kushinda bao 1-0 mbele ya Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Kaitaba.
KMC ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 36 huku Kagera Sugar ikiwa nafasi ya nane na pointi zake 44.
Anwary Binde, Ofisa Habari wa KMC amesema kuwa walipoteza mechi yao mbele ya Biashara United, hivyo watapambana mbele ya Kagera Sugar kupata pointi tatu.
"Mchezo wetu dhidi ya Biashara tulifungwa kutokana na makosa tuliyofanya na tuliikuta timu ikiwa nyumbani hivyo ushindani ulikuwa mkubwa kwa timu zote.Hayo yamepita tunatazama mchezo wetu wa leo.
"Hautakuwa mchezo mwepesi kwani kila timu imejipanga kupata matokeo chanya, tupo vizuri katika maandalizi tunaamini tutapata ushindi.
"Kwa sasa kila timu inapambana kufikia malengo yake nasi pia tunapambana kuyafikia malengo yetu hivyo ni wakati wetu kupata kile ambacho tunakihitaji," amesema.
Mtupiaji namba moja ndani ya Kagera Sugar, Yusuph Mhilu akiwa na mabao 12 kibindoni amesema kuwa watapambana kwenye mechi zao zote kupata matokeo mazuri.
0 COMMENTS:
Post a Comment