WACHEZAJI wa Klabu ya Liverpool inayonolewa na Jurgen Klopp wameshangilia kwa pamoja ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kutangazwa kuwa Mabingwa rasmi.
Mara ya mwisho Liverpool kutwaa taji hilo ilikuwa ni mwaka 1990, walisubiri kutwaa taji hilo baada ya kupita miaka 30.
Klopp akiwa hotelini na rafiki zake alikuwa akiutazama mchezo wa Manchester City wakati ikipokea kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Chelsea kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Stamford Bridge ambao ulithibitisha kuwa Liverpool ni mabingwa rasmi.
Wachezaji na kocha wote walikuwa wakishangilia ubingwa huo wakiwa nyumbani, huku Jordan Henderson ambaye ni nahodha naye ameonekana kuwa na furaha kwa timu yake kutwaa taji hilo kubwa.
Van Dijk beki kisiki wa Klabu hiyo akiwa na wachezaji wenzake pia alionekana akishangilia bao la penalti lilifungwa na Willian dakika ya 78 na lile la kwanza lilifungwa na Christian Pulisic dakika ya 36 huku lile la Manchester City likifungwa na Kevin De Bruyne.
Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah alituma video yake akishangilia huku akiimba nyimbo kutokana na furaha ya ubingwa ambao wameutwaa wakiwa na pointi 86 baada ya kucheza mechi 31 ambazo hazitafikiwa na City iliyo nafasi ya pili na pointi zake 63.
Mchezo wake unaofuata Julai,2 Liverpool itamenyana na Manchester City, Uwanja wa Etihad.
0 COMMENTS:
Post a Comment