July 18, 2020


KLABU ya Simba imeeleza kuwa licha ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, wanahitaji rekodi zaidi kwa kutwaa Kombe la FA, ili kuweza kupata makombe matatu ndani ya msimu mmoja ikiwemo na Ngao ya Jamii.

Simba ambayo tayari imeshafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kwa kufikisha pointi ambazo timu yeyote haitazifikia hata baada ya mechi zilizobaki kumalizika, inahitaji kutwaa Kombe la FA iwe isiwe ili kuweza kuweka rekodi msimu huu ya kutwaa makombe matatu ambapo hadi sasa wanayo mawili la Ngao ya Jamii na ligi kuu.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema kuwa, wamepata furaha kuona wamefanikiwa kuwafunga watani wao Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA na sasa kilichobakia ni kuweka rekodi ya kuhakikisha wanamaliza msimu kwa kutwaa makombe matatu pamoja na kufunga idadi kubwa ya mabao.

"Ni furaha kuona tumefanikiwa kuwafunga wapinzani wetu, tuliwapa mapumziko wachezaji baada ya mchezo dhidi ya Yanga, sasa tunaanza maandalizi ya ligi tunahitaji kumaliza kwa kuweka rekodi ya kupata pointi nyingi ligi kuu pamoja na kufunga mabao mengi.

“Pia tunahitaji rekodi ya kutwaa makombe matatu ndani ya msimu huu kwani hatujawahi kuwa na makombe matatu ndani ya msimu mmoja, tumefanikiwa kutwaa Kombe la Ngao ya Jamii, ligi kuu na sasa tunakwenda kupambania kulipata Kombe la FA ili tuweze kuweka rekodi.

“Mechi ya fainali ya FA itakuwa ya ushindani sana kwani kila timu itakuja kitofauti katika mchezo huo, Namungo ipo nafasi ya nne kwenye ligi, hivyo hatubweteki kuwaona kama timu ya kawaida kwani na yenyewe inahitaji kuweka rekodi na sisi tunahitaji hiyo rekodi zaidi yao, tunajipanga kwa kuhakikisha tunakwenda kupambana ili mwisho wa siku tushinde,” amesema.

Namungo iliyo chini ya Kocha Mkuu, Hitimana Thiery iliibukia kwenye fainali baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Sahare All Stars Uwanja wa Mkwakwani.

Fainali inatarajiwa kuchezwa Agosti 2, Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic