KWA mara ya kwanza, beki mpya wa Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto aliliripoti na kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake tayari kwa ajili ya kuanza msimu mpya wa 2020/2021.
Mwamnyeto ni kati ya wachezaji wapya wazawa waliosajiliwa na timu hiyo katika kuelekea msimu ujao wengine ni Zawadi Mauya, Yassin Mustapha, Waziri Junior, Kibwana Shomari, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Farid Mussa.
Timu hiyo Jumatatu ya wiki hii ilianza mazoezi yake ya pamoja kujiandaa na msimu mpya kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Ubungo jijini Dar es Salaam chini ya kocha msaidizi, Riedoh Berdien raia wa Afrika Kusini ambapo Mwamnyeto alitumia zaidi ya dakika 120 kufanya mazoezi.
Akizungumza na Championi Ijumaa,Meneja Mkuu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema Mwamnyeto aliripoti jana Alhamisi sambamba na kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake.
Alisema kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa wote wameripoti mazoezini isipokuwa Farid Mussa pekee ambaye yeye alisajiliwa juzi Jumatano na kutambulishwa na uongozi wa timu hiyo.
“Kati ya wachezaji wazawa ambaye bado hajaripoti ni Farid ambaye yeye ana ruhusa maalum kutoka kwa uongozi ambaye huenda akajiunga na wenzake kuanzia kesho Ijumaa (leo),” alisema Saleh.
0 COMMENTS:
Post a Comment