KESHO
Jumapili, tunatarajia kushuhudia mchezo wa mwisho kwa msimu huu wa soka wa
2019/20 Tanzania Bara. Kumbuka msimu huu ulianza Agosti, 2019.
Mchezo huo
wa kufunga msimu huu utakuwa ni wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam
maarufu Kombe la FA utakaozikutanisha Namungo FC dhidi ya Simba SC.
Katika
Uwanja wa Nelson Mandela kule Sumbawanga mkoani Rukwa, ndipo mchezo huo
utachezwa na kumpata bingwa mpya wa michuano hiyo.
Kila upande
umekuwa ukijinasibu kuibuka na ushindi, Simba wamepania kushinda huku wakitaka
kuchukua taji la tatu msimu huu, Namungo wao wanataka kuchukua taji hilo na
kuweka heshima.
Namungo
msimu huu kwao ni wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara, wamefanya vizuri katika ligi
na kumaliza nafasi ya nne ikiwa na pointi 64. Simba ni mabingwa wakikusanya
pointi 88. Timu zote zilicheza mechi 38.
Katika ligi,
timu hizo zimekutana mara mbili, Simba imeibuka wababe kwa kushinda mechi moja
na sare moja, hivyo Namungo wana muda wa kujiuliza hapo kesho.
Binafsi
nautazama mchezo huu kama mmoja kati ya mchezo ambao utakuwa wa kuvutia sana
kutokana na timu zinazokwenda kukutana hapo kesho.
Kitendo cha
Namungo kupanda daraja, kisha kumaliza ndani ya nne bora kwenye ligi si cha
kubeza. Hii inanikumbusha KMC ya msimu wa 2018/19 ambayo ilikwenda kushiriki
Kombe la Shirikisho Afrika.
Namungo
wanaonekana kujipanga kufanya kweli, katika hilo wameanza kufanikiwa kwenye
ligi, kazi iliyobaki sasa ni katika mchezo huo wa kesho kuona wanamaliza kazi.
Kocha wao,
Hitimana Thiery, amewazungumzia Simba akisema licha ya kwamba ni mabingwa wa
ligi, haimaanishi wao wataingia kinyonge, wanawaheshimu kwanza, lakini mambo
mengine yatafuata.
Simba nao
kupitia kwa kocha wao, Sven Vandenbroeck, amesema anawaheshimu Namungo na
anaona mchezo utakuwa mgumu, lakini wanajipanga kushinda.
Kila mmoja
anataka kushinda, hapo ndipo utaona namna gani mchezo huu utakuwa mgumu, lakini
angalizo ni kwamba, waamuzi waliopewa dhamana ya kusimamia mchezo huu,
wazitafsiri vema sheria 17 za soka.
Tunataka
kuona mchezo wa haki, hatutaki kusikia baada ya mchezo kwamba kuna timu
imependelewa, hiyo haitaleta picha nzuri kabisa.
Atakayeshinda
ashinde kwa uwezo wake au kwa bahati kwa sababu tunatambua kwamba kwenye soka
kuna ishu ya bahati au uwezo.
Timu inaweza
kuwa na uwezo mkubwa, lakini ikakosa bahati, ikapoteza mchezo, lakini wakati
mwingine timu inakuwa na hivyo vyote, hapo inakuwa rahisi kuibuka na ushindi
tena mnono.
Ikiwa ni
mchezo wa mwisho wa kufunga msimu huu, tunataka kuona kila upande ukionesha
ujuzi wake ule ambao kila mmoja ataufurahia kwa maana ya mashabiki na
watazamaji kwa jumla.
Wale
watakaokuwa uwanjani na watakaoshuhudia mchezo kupitia runinga, wanataka kuona
soka la ufundi na sio butuabutua.
Wachezaji
kumbukeni kipindi kijacho ni cha usajili, mnaweza kuutumia vema mchezo huu
kujiuza, hivyo nafasi hii itumieni vema.
0 COMMENTS:
Post a Comment