STRAIKA wa kutumainiwa wa kikosi cha timu ya Waandishi wa Habari za Michezo Wanawake Tanzania Bara, Lucy Mgina (Chicharito), amefunguka kuwa wanahitaji kuweka historia ya kuwafunga timu ya Wachezaji Wanawake wa Ligi Kuu Bara katika mchezo wa hisani utakaochezwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Karume, Dar.
Chicharito amesema wao kama wanahabari wanahitaji kuwaonyesha Watanzania kuwa, mbali ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuandika na kutangaza masuala ya michezo, pia wana uwezo mkubwa wa kulisakata soka na watahakikisha wanawafunga nyingi wapinzani wao hao.
Lucy ambaye ni Mhariri wa Gazeti la Championi Jumamosi ameeleza kuwa, yeye binafsi atafunga mabao siyo chini ya matatu na hiyo inatokana na uwezo wake mkubwa anaonyesha katika mazoezi anayofanya kila siku asubuhi na jioni. Mgina ambaye pia anajulikana kwa jina la Nicki Minaj alitamba kuwa: “Lazima tuwachape wale vijana na kuweka historia kwenye nchi hii, tunajua wapinzani wetu bado wapo kwenye moto kwa kuwa wametoka kumaliza ligi yao juzi tu."
Waandishi wa Habari za Michezo Wanawake wameandaa mchezo huo kwa lengo la kulitangaza na kulipa thamani soka la wanawake nchini, ambapo wadau mbalimbali na viongozi wa ngazi za juu serikalini wanatarajia kuhudhuria mchezo huo ikiwa kama sehemu ya kuunga mkono jitihada hizo.
Baadhi ya wachezaji wanaounda kikosi cha Wanahabari FC ni kipa Martha Mboma, ambaye ni Mhariri wa Spoti Xtra, Mwanaidi Suleiman, Devotha Kihwelo, Victoria Mungure, Salama Van Ngale, Ester Maongezi, Fatma Likwata, Pendo Kamba, Salma Seif, Diana Songa na nyota wengine.
Huku kikosi cha wanasoka kikiundwa na Mwanahamisi Omary (Gaucho), Julietha Singano, Fatma Hassan, Irene Kisisa, Irene Matowo, Najiath Idrisa, Fatuma Khatibu, Joelle Bukuru, Protasia Mbunda, Amina Ally, Opah Clement, Asha Djafar na nyota wengine kibao.
opa kashawafunga waandishi wa habari vibonge
ReplyDelete