August 21, 2020

 








x

Na Saleh Ally

UMESIKIA mara nyingi sana timu za mikoani zikilalamika kutokuwa na fedha na zikasema haziwezi kusajili wachezaji wazuri kwa kuwa hazina fedha ya kutosha.

 

Timu nyingi zinatokea katika miji mikubwa, mfano Mwanza au Arusha au Mbeya lakini utaona zinalia kuhusiana na fedha jambo ambalo linaonekana kuwa ni ugonjwa sugu.

 

Unaweza ukajiuliza, timu inayotokea katika jiji kama la Mwanza, timu ambayo inawasogezea Mwanza burudani ya Ligi Kuu Bara inaweza vipi kukwama na kushindwa kupata hata fedha ya usajili na baadaye ikawa shida fedha ya uendeshaji!

 

Haya mambo yamekuwa kwa muda mrefu sana, ndio maana timu ambazo zimekuwa na gumzo kubwa katika masuala ya usajili imebaki kwa Yanga na Simba pamoja na Azam FC ambazo zote za jijini Dar es Salaam.

 

Ni aghalabu sana kuona timu ya mikoani ikitikisa kwa usajili na kufanya vizuri kama ilivyokuwa wakati ule enzi za Pamba ya Mwanza, Mecco ya Mbeya, CDA ya Dodoma na nyinginezo.

Wakati huo, kila utakayemuuliza, atakuambia kuwa hii ilitokana na yale makampuni yaliyokuwa yakizimiliki timu hizo na kutoa huduma sahihi zikawa bora.

 

Jiulize kwa nini kwa sasa mashirika hayataki kufanya hivyo? Kawaida kutakuwa na kasoro kwa kuwa faida haikuwa kubwa sana. Lakini kuna jambo la kujifunza kwamba, je, Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma na kwingineko hawana makampuni ya kuendesha timu?

 

Sawa, hakuna makampuni, basi tujiuliza hakuna hata makampuni ya kuzidhamini hizo timu ambazo zinasafiri kucheza nchi nzima kucheza Ligi Kuu Bara na zitaweza kuzitangaza kampuni hizo?

 

Kwangu nitakuwambia kampuni hizo zipo, lakini kuna tatizo kubwa kwa viongozi wanaoziongoza timu hizo za mikoani kutokana na kuamini wanajua mambo mengi lakini hawajui.

 

Timu nyingi za mikoani haziendeshwi kwa weledi  na bahati mbaya viongozi wamejisahau kwa baadhi ya timu nyingi za mikoani wanataka kuziendesha kwa mfumo kama ule wa Simba na Yanga na mwisho wanakwama.

 

Pia ndani ya timu hizo, kuna viongozi wana itikadi za Uyanga na Usimba, wako tayari hata kuzisaliti timu zao inapofikia wakati wanakutana na Yanga au Simba, hii si sawa na imekuwa hatari sana kwa afya za timu hizo na mfano mzuri, Toto African ya Mwanza imekuwa sehemu ya wahanga wa hili jambo, leo iko mafichoni katika ramani ya soka nchini.

 

Katika timu za mikoani ni lazima kabisa viongozi waachane kabisa na mambo kadhaa niliyoyataja yakiwemo yale mambo yanayoziumiza timu zao kama mifumo kama Simba na Yanga au wao kugeuka mashabiki wa klabu hizo kubwa za Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.

Wafanye kazi zao kwa maisha ya klabu zao na kuzipatia mafanikio. Watengeneze mipango mikakati ya kuanzia ngazi ya chini, kati na juu kwa maana ya kuhakikisha utekelezaji wake unaleta mabadiliko.

 

Watengeneze nidhamu ya juu na mbinu za masoko kuwashawishi wadhamini wanaokuwa katika mikoa yao ili washawishike kutangaza nao.

 

Wakati wakijitangaza, wao wataingiza fedha ambazo zitawasaidia kusajili wachezaji wazuri ambao wataongeza uimara wa timu na kusaidia timu za mikoa nazo kuweza kupambana na timu za Dar es Salaam ili kuepusha kuonekana ubora umebaki Dar es Salaam pekee na timu za mikoani ni wasindikizaji.

 

Kama watafanya mambo kwa uhakika, usajili bora, mipango sahihi ya masoko, basi hata mashabiki nao watashawishika kuziunga mkono timu zao kwa kuingia kwa wingi uwanjani, kununua jezi na vifaa kadhaa na baada ya muda zitakuwa bora sana na zenye uwezo wa kifedha.

 

Mikoani wanaweza kuleta mabadiliko ya mpira wa Tanzania ukahamia hadi mikoani na si kubaki Dar es Salaam tu. Itakuwa hivyo, wakiamua.

2 COMMENTS:

  1. Mr Salehe Ally hv unategemea Kama watu wa Yanga na Simba wanajipenyeza kwa kugombea Mikoani wapate Uwakilishi kwenye Mkutano mkuu wa TFF lengo ikiwa ni kuwa na wajumbe wengi wenye mlengo mmoja wa Simba au Yanga kimaslahi,usitegemee wawe na mtizamo wako .Ndiyo maana tunasema hapa ni Sera za Nchi zinatakiwa na TFF wawe wakali hasa kwenye huu Uongozi wa vyama vya Mikoani watu siyo Wazalendo akili yote ipo Simba na Yanga ,wewe Hilo chunguza mpaka Team zinashuka kisa Simba na Yanga eg Lipuli,Toto Africa nk

    ReplyDelete
  2. Na wenye tatizo ni Tff cse wasingeruhusu hilo Timu zingekuwa juu,inashangaza Team Kama hiyo ulioweka hapo juu , siku hizi imekuwa ya Kiswahili Wahuni wameivamia sasa HV hata mwelekeo wa usajili wameanza kuokoteza

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic