MABINGWA wa kihistoria katika Ligi Kuu Bara, Yanga, leo Jumapili wana kazi moja tu ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi mbele ya Mtibwa Sugar, ikiwa ni baada ya kutoka kuwachapa ndugu zao, Kagera Sugar bao 1-0.
Mtibwa wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Jamhuri mkoani Morogoro, leo watakuwa wenyeji wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Msimu huu, Mtibwa bado haijapoteza mechi yoyote ya nyumbani ambapo hivi karibuni ilitoka kuikazia Simba uwanjani hapo na kutoka sare ya 1-1.
Yanga itaingia uwanjani hapo ikitaka kuionesha Simba kwamba wao walishindwa kuifunga Mtibwa kwa uzembe wao, hivyo wakae kwa kutulia kushuhudia burudani na soka safi kutoka kwao litakalochagizwa na ushindi murua.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana uwanjani hapo, matokeo yalikuwa 1-1.
Sasa kuelekea mchezo wa leo, winga wa Yanga, Tuisila Kisinda, ameibuka na kusema: “Waleteni hao Mtibwa tuwanyooshe, uwanja si tatizo kwangu.”
Wakati Kisinda akisema hivyo, Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila, amesema: “Nimekiandaa vema kikosi changu, kipo imara kabisa, hakuna majeruhi hata mmoja, kuna mikakati mingi tumeipanga kuhakikisha tunashinda.
“Tumewasoma wapinzani wetu, tunafahamu Yanga ni timu nzuri, lakini hata sisi tuna kikosi kizuri pia na tunachohitaji ni pointi tatu dhidi yao.”
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema jana asubuhi walifanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Jamhuri, tayari kwa ajili ya kuwavaa Mtibwa wakiwa na morali ya juu huku wachezaji wote wakiwa fiti isipokuwa Mapinduzi Balama anayeendelea na matibabu.
Beki wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anaitumikia Mtibwa Sugar, Hassan Kessy, amesema yupo sawa kuwakabili waajiri wake hao wa zamani.
“Ligi ni ngumu, timu zimejipanga sana na kuna ushindani, kwa upande wangu nipo tayari kuwakabili ingawa suala la kucheza mwalimu ndiye anayejua,” alisema Kessy.
Rekodi zinaonesha kuwa, timu hizo tangu mwaka 2011, zimekutana mara 18 ndani ya Ligi Kuu Bara. Yanga imeshinda mechi nane, sare sita na Mtibwa imeshinda mechi nne.
Yanga haina rekodi nzuri ndani ya Uwanja wa Jamhuri inapocheza na Mtibwa, kwani katika mechi tisa, imeshinda moja pekee. Mtibwa imeshinda nne na sare nne.Hivyo basi, kwa rekodi hizi, mtu leo hatoki salama, lolote linaweza kutokea.
0 COMMENTS:
Post a Comment