September 13, 2020


 KAZI ndiyo imeanza kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Zlatko Krmpotic raia wa Serbia kuirudisha timu hiyo kwenye furaha kwa kuanza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao wameukosa kwa misimu mitatu mfululizo.

Ushindani ndani ya ligi kwa msimu wa 2020/21, unaonekana ni mkubwa kwa kuwa timu zimefanya usajili kwa malengo na hesabu kubwa ni kupata ushindi.

 

Mechi za raundi ya kwanza zilikamilika kwa kupatikana mabao 14 jambo linaloonesha ushindani msimu huu utakuwa mkubwa.Kwa upande wa Yanga, tayari Krmpotic ameanza kuonja kukaa benchi na kushuhudia timu yake ikiambulia pointi moja mbele ya Tanzania Prisons, ilikuwa Septemba 6 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.


Leo, Septemba 13 uwanjani hapo ana kibarua mbele ya Mbeya City.Spoti Xtra linakuletea mechi kumi zijazo za Yanga ambazo ni sawa na dakika 900 ambazo zitampa kocha huyo picha ya kile anachokitaka.Katika mechi hizo, tunaangalia na namna msimu uliopita matokeo yalikuwaje pindi walipokutana:-

 

YANGA V MBEYA CITY

Mbeya City, ikiwa na hasira za kunyooshwa mabao 4-0 na KMC, leo itakutana na Yanga.Rekodi zinaonyesha kuwa kupata pointi tatu kwa Mbeya City shughuli yake sio nyepesi kwani msimu uliopita mechi zote mbili timu hizo ziligawana pointi mojamoja. Hakuna iliyoibuka na ushindi.


Mechi ya kwanza iliyochezwa mkoani Mbeya, matokeo yalikuwa 0-0, kisha mechi ya pili jijini Dar ilikuwa 1-1. Yanga wanaweza kushinda.


KAGERA SUGAR V YANGA

Baada ya kucheza mechi mbili nyumbani, hii itakuwa mara ya kwanza Yanga inakwenda ugenini mkoani Kagera kupambana na Kagera Sugar.Mechi hiyo itachezwa Septemba 19 kwenye Uwanja wa Kaitaba.


Msimu uliopita timu hizo zilipokutana Uwanja wa Uhuru, Dar, Kagera Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, kule Kaitaba Yanga ikashinda 1-0. Mechi hii itakuwa ya ushindani mkubwa, inaweza kuwa sare.

 

MTIBWA SUGAR V YANGA 


Septemba 27 Yanga itakuwa Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar.Mchezo wa kwanza msimu uliopita, Yanga ikiwa nyumbani iliifunga Mtibwa bao 1-0, mechi ya pili kule Jamhuri matokeo yalikuwa 1-1.


YANGA V COASTAL UNION

Vijana wa Juma Mgunda, Coastal Union watakutana na nahodha wao wa zamani, Bakari Mwamnyeto ambaye kwa sasa anakipiga ndani ya Yanga. Mechi itakuwa Oktoba 3 kwenye Uwanja wa Mkapa.


Msimu uliopita mchezo wa kwanza uliochezwa Uhuru, Yanga ilishinda bao 1-0. Mchezo wa pili Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ngoma ilikuwa 0-0. Safari hii Coastal inaonekana kuwa si ya moto sana, inaweza kupoteza mechi hii.

 

YANGA V POLISI TANZANIA

Oktoba 11 kwenye Uwanja wa Mkapa, Yanga itawakaribisha Polisi Tanzania. Rekodi zinaonesha mchezo wa kwanza kwa msimu uliopita uliochezwa Uwanja wa Uhuru, matokeo yalikuwa 3-3.Mechi ya pili iliyochezwa Uwanja wa Ushirika, Moshi, ngoma ilikuwa 1-1. Safari hii sare pia inaweza kupatikana.


YANGA V SIMBA

Watani hawa wa jadi, watakutana kwa mara ya kwanza msimu huu Oktoba 18 kwenye Uwanja wa Mkapa.Msimu uliopita mchezo wa kwanza uliopigwa Januari 4, ulimalizika kwa sare ya 2-2, mechi ya pili Yanga ikashinda 1-0.Mpaka sasa bado kuna asilimia za kupatikana kwa sare kwenye mchezo huo, lakini itategemea na hali za vikosi hivyo kutoka leo hadi siku ya mchezo. Lolote linaweza kutokea.

 

BIASHARA V YANGA

Novemba Mosi, Yanga itakuwa mkoani Mara kucheza na Biashara United kwenye Uwanja wa Karume.Ile mechi ya kwanza msimu uliopita iliyochezwa Uwanja wa Mkapa, Yanga ilishinda 1-0, marudiano ikawa 0-0.


GWAMBINA V YANGA


Hii itakuwa ni mara ya kwanza Yanga kukutana na Gwambina ambayo imepanda daraja. Mechi itachezwa jijini Mwanza.Timu hizo zikiwa zinakutana Novemba 7, Yanga itaenda kupambana na kocha wao wa zamani, Mwinyi Zahera ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi la Gwambina. Ngoma ngumu hii.


AZAM V YANGA

Itakuwa ni balaa lingine Novemba 15 atakalokutana nalo Krmprotic. Msimu uliopita mchezo wa kwanza Yanga ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na mchezo wa pili walitoshana nguvu ya bila kufungana.


Safari hii kila timu imejiimarisha, dakika tisini zitaamua nani mshindi ingawa sare inaweza kuwa ni matokeo yanayoweza kutokea.

 

YANGA V NAMUNGO

Novemba 22, Namungo yenye maskani yake Lindi, itakutana na mziki wa Yanga, Uwanja wa Mkapa.Msimu uliopita mchezo wa kwanza ulichezwa Uwanja wa Majaliwa, Lindi, matokeo yalikuwa 1-1. Mchezo wa pili jijini Dar, ikaisha tena kwa sare ya 2-2. Safari hii, inaweza kujirudia matokeo hayo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic