October 3, 2020

 


MOTO Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2020/21 unazidi kupamba moto huku ile vita ya tano bora ikiwa imeanza kuonekana mwanzoni kabisa.

KMC yenye maskani yake pale Kinondoni ilianza kwa kasi ya ajabu na iliongoza raundi tatu huku ikiwaburuza vigongo Yanga na Simba imeshushwa raundi ya nne baada ya kupoteza mbele ya Kagera Sugar kwa kufungwa bao 1-0.

Azam FC ndio iliwashusha KMC kwa sasa ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 12 inaonekana wana jambo lao kwa msimu wa 2020/21 baada ya msimu wa 2019/20 kumaliza ligi wakiwa nafasi ya tatu na pointi zao 70 baada ya kucheza mechi 38 msimu huu wameanza namna hii twende sawa:-

 

Viwanja  vyote wanapeta

Wakiwa wametumia viwanja vitatu na muda tofauti wameendeleza ubabe wao wa kusepa na pointi tatu.

Uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex walicheza mechi mbili na zote zilipigwa majira ya saa 1:00 usiku walishinda mbele ya Polisi Tanzania bao 1-0, Coastal Union 0-2 na kujikusanyia pointi tatu.

 Walipotoka nje ya Azam Complex wamecheza mechi mbili, moja Uwanja wa Sokoine mbele ya Mbeya City 0-1 majira ya saa 8:00 na ile ya nne ilikuwa Uwanja wa Nelson Mandela ilishinda bao  1-0 mbele ya Tanzania Prisons majira ya saa 10:00 jioni.

Prince Dube

Nyota yake ni kali ndani ya ardhi ya Bongo ambapo mechi yake yake ya kwanza ya ligi mbele ya Polisi Tanzania alianza kwa kutoa pasi ya bao kwa kumpa mshikaji wake Obrey Chirwa wakati Azam ikishinda bao 1-0.

Hakuishia hapo alipachika mabao mawili mbele ya Coastal Union na bao moja mbele ya Tanzania Prisons.

Cioaba awazidi ujanja wote

Aristica Cioaba, Kocha Mkuu wa Azam FC amewazidi ujanja makocha wote ndani ya Ligi Kuu Bara ikiwa ni pamoja na Sven Vandenbroek wa Simba ambao ni mabingwa watetezi.

Raundi zote nne akiwa kwenye benchi amekusanya pointi 12 akiwa hajaonja joto ya kufungwa wala kuonja sare ndani ya uwanja huku Simba ikiwa imeonja sare ya kufungana bao 1-1 mbele ya Mtibwa Sugar na Yanga ya Zlatko Krmpotic ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 mbele ya Prisons.

Ukuta wao matata

Ndani ya ligi kuu bara, ukuta wa Azam FC unaoundwa na beki bora kwa msimu wa 2019/20, Nicolas Wadada ambaye alipiga jumla ya pasi nane za mabao na kufunga bao moja kati ya 52 msimu uliopita haujaruhusu kufungwa bao mpaka sasa.

Wadada ameupoteza ukuta wa Mbeya City inayonolewa na Kocha Mkuu, Amri Said ambao umefungwa jumla ya mabao saba ndani ya uwanja.

Kissu awa mtamu

Kipa wao namba moja David Kissu ambaye ni ingizo jipya kutoka Klabu ya Gormahia ameanza vizuri maisha yake ndani ya Azam FC ambapo amecheza mechi nne na kuyeyusha dakika 360 bila kuokota mpira nyavuni mwake.

Hesabu zao hizi hapa

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin, Popat ameliambia Spoti Xtra kuwa malengo makubwa ni kuona timu inakuwa na mwendelezo mzuri utakaowapa mataji.

“Tunakikosi kizuri ambacho kinapata matokeo kwenye mechi zetu hilo ni jambo jema. Malengo yetu ni kuona kwamba tunaweza kutwaa taji la ligi na kurejea kwenye michuano ya kimataifa.”

Hawa hapa watupiaji wake

Azam FC kwenye mechi zake nne ilizocheza kwa msimu wa 2020/21 imekusanya jumla ya mabao matano ambayo yamefungwa na washambuliaji wake wawili na kiungo mmoja.

Obrey Chirwa alifunga bao moja mbele ya Polisi Tanzania, Prince Dube alifunga mabao matatu mbele ya Coastal Union mawili na mbele ya Tanzania Prisons bao moja huku Ally Niyonzima akitupia bao moja ilikuwa mbele ya Mbeya City.

Matokeo yake:-Azam FC 1- 0 Polisi Tanzania, Azam FC 2-0 Coastal Union, Mbeya City 0-1 Azam FC na Tanzania Prisons 0-1 Azam FC.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic