NA. Leen Essau
MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, Saleh Ally ‘Saleh Jembe’ ametamba kuwa vijana wake wataibuka na ushindi mnono dhidi ya Azam Media FC katika mchezo mkali wa kirafiki utakaopigwa leo Jumamosi, Dar, Uwanja wa Karume.
Jembe ambaye ni mshambuliaji wa kutegemewa kikosi cha kwanza cha timu namba moja kwa ubora ndani ya Bongo kwa Vyombo vya Habari amesema wakati wake sasa ni kuona anakaa kwenye benchi la ufundi akiwa ni mshauri mkuu.
“Mimi nitakuwepo kwenye benchi la ufundi leo kwani nimecheza mechi nyingi kwa hiyo nimeamua kukaa kwenye benchi kwa heshima ili kuwashuhudia vijana wangu wakipambana mbele ya Azam Media.
"Niwe muwazi kabisa na ninapenda kusema ukweli, Azam Media ni miongoni mwa timu ambazo zipo vizuri na zina vijana wengi ambao wanapenda mpira na wanacheza mbali na kuutangaza pamoja kuuandika.
"Vijana wangu ninawaambia na nimewaambia kwamba wasifikiri wanakwenda kucheza na timu zile ambazo wamezoea kufunga mabao mengi wanakutana na muziki mwingine nami nitakuwepo pia," amesema.
Alwatan Ngoda mchezaji wa kutumainiwa ndani ya Azam Media amesema kuwa maandalizi yao yapo vizuri na wataingia uwanjani kwa heshima kusaka ushindi kwenye mchezo huo.
"Ni mchezo mgumu na una ushindani ila kwa namna ambavyo tumejipanga kiujumla, namna ambavyo wafanyakazi wameipokea taarifa, utakuwa ni mchezo mzuri na wenye ushindani mkubwa," amesema.
Mchezo wa leo ni maalumu kwa ajili ya kuendeleza hamasa kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kesho, Uwanja wa Mkapa kuipa sapoti timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo itacheza na Burundi.
Hautakuwa na kiingilio utachezwa majira ya saa 10:00 jioni, makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).
0 COMMENTS:
Post a Comment