KESHO Jumapili, timu yetu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itakuwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ni sehemu
ya kukiandaa kikosi kuelekea michezo ijayo ya kimashindano ikiwemo kufuzu Afcon
na Kombe la Dunia 2022.
Tunapocheza mechi za
kirafiki ni sehemu ya kukiandaa kikosi kuwa imara na cha ushindani hivyo hizi
mechi zina umuhimu wake mkubwa.
Taifa Stars ambayo
kwenye viwango vya soka kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA)
hatupo sehemu nzuri, tunapaswa kuendelea kufanya vizuri ili kupanda viwango.
Kufanya huko vizuri
kunategemewa na sapoti ya Watanzania wote, hivyo hatuna budi kesho kwenda kwa
Mkapa kuwapa sapoti vijana wetu.
Tumeona benchi la
ufundi chini ya kocha mkuu, Etienne Ndayiragije likiita kikosi ambacho hakuna
aliyekuwa na maswali mengi.
Kikosi kimezingatia
viwango husika vya wachezaji kutokana na kile walichokifanya ndani ya muda huu.
Kikubwa ambacho
kinazidi kukipa nguvu kikosi hiki ni uwepo wa nyota wa kimataifa walioitwa
ambao wote wamefika kwa wakati kasoro kiungo, Himid Mao ambaye alikuwa na
majukumu katika klabu yake ya ENPPI ya Misri.
Kabla ya mchezo huu,
niliwahi kusikia watu wakizungumza tofauti juu ya timu tunayokwenda kucheza
nayo kwamba inaweza isiwe kipimo sahihi kwetu. Mimi napingana nao.
Napingana nao kwa
sababu licha ya kwamba Burundi tumewapita kwenye viwango vya soka duniani,
lakini ukiangalia vikosi pengine wao wametuzidi kwa wachezaji wanaocheza nje ya
nchi yao.
Kikosi chao ukiangalia
kina nyota watatu wanaocheza soka hapa Tanzania ambao ni Jonathan Nahimana,
Blaise Bigirimana na Steve Nzigamasabo wanaokipiga Namungo.
Nahodha wao ni Saido
Berahino anayecheza Zulte Waregem ya Ubelgiji.
Wengine ni Cedric
Amissi (Al-Taawoun, Saudi Arabia), Mohamed Amissi (Heracles Almelo, Ubelgiji),
Philip Nzeyimana Oslev (Akademisk Boldklub Gladsaxe, Denmark), Frederick
Nsabiyumva (Chippa United, Afrika Kusini), Bonfils Caleb Bimenyimana (Pohronie,
Slovakia), Yussuf Nyange Ndayishimiye (Yeni Malatyaspor, Uturuki) na Abdoul
Razzak Fiston wa ENPPI ya Misri.
Hao ni wachezaji 11,
huku kwetu tunao sita ambao ni Himid Mao (ENPPI SC, Misri), Ally Msengi (Stellenbosch
FC, Afrika Kusini), Mbwana Samatta (Fenerbhace FC, Uturuki), Thomas Ulimwengu
(TP Mazembe DR Congo), Nickson Kibabage na Simon Msuva wanaocheza Diffa El
Jadidi, Morocco).
Ukiangalia vizuri
utagundua kwamba Burundi itakuwa kipimo sahihi kwetu kutokana na sababu hizo
nilizozieleza.
Hivyo basi twendeni
uwanjani kuwapa sapoti vijana, ule ushabiki wetu wa klabu tuuweke pembeni kisha
tuungane kwa pamoja kuishangilia Taifa Stars.
Siku zote kwenye soka
shabiki ni mchezaji wa 12, hivyo uwepo wake kunaleta nguvu zaidi kwa wachezaji
waliopo ndani ya uwanja wanaoipeperusha bendera ya nchi yetu.
Kufanya vizuri kwa
Taifa Stars kunahitaji nguvu zetu kwa hamasa ya kuwashangilia ili watupe
tunachokitaka.
Tukiwasusia wanaweza
kushindwa kufikia malengo na hapo hakutakuwa wa kumlaumu.
Tuiunge mkono Taifa
Stars, tunapoenda uwanjani tuvae jezi na kuupendezesha uwanja kwa rangi za
taifa letu.
Hiyo itawafanya
wapinzani waone Watanzania tumeamua na tunaipenda timu yetu. Hivyo tuhamasishane
kwenda kuwasapoti vijana wetu.
Mech itaanza muda gan?
ReplyDelete