October 9, 2020


 OKTOBA 11 Uwanja wa Mkapa kuna kazi moja kubwa kwa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kupambana kwa ajili ya Taifa kucheza mchezo wa kirafiki ambao upo kwenye kalenda ya Fifa.

Mchezo huo ni dhidi ya jirani zetu ambao ni Burundi hivyo hautakuwa mchezo mwepesi ukizingatia kwamba una maana kubwa kwenye maendeleo ya soka letu la Tanzania.

Ninaona kwamba Watanzania ambao ni mashabiki wakubwa wa timu ya Taifa ya Tanzania kwa hivi karibuni wamekuwa na kasumba ya kutengeneza makundi na matabaka hasa kwa upande wa kushangilia timu zao.

Wapo pia mashabiki ambao wamepewa adhabu ya kutokwenda kwenye mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na zile nyingine kutokana na kufanya vurugu ndani ya uwanja kwa wapinzani wao.

Ugonjwa huu ni mbaya na ni tatizo ambalo kama litaendelea kwenye mechi ambazo zinachezwa litasababisha matatizo makubwa zaidi ya haya ambayo yanaonekana kwa sasa.

Kuna umuhimu wa mashabiki ndani ya uwanja na kuna umuhimu wa ulinzi wa mashabiki ndani ya uwanja. Mlinzi wa kwanza wa shabiki ni shabiki mwenyewe hivyo kila mmoja kwa sasa anajukumu la kuwa mlinzi wa mwenzake.

Nimeamua kuanza namna hii kwa sababu kuna mashabiki ambao wao ishu yao kubwa ni kwenye aina ya rangi ambayo wanakutana nayo pindi wawapo uwanjani.

Hofu yangu isije ikatokea kwamba ule ugonjwa wa rangi ukatokea tena Oktoba 11 wakati Taifa Stars itakapokuwa ikicheza na Burundi. Hapana katika hili tusifanye hivyo tena.

Tupo kwenye wakati wa mapambano kwa ajili ya ujenzi wa taifa letu la Tanzania kwenye medali za michezo kitaifa na kimataifa tusiruhusu dosari kujitokeza kwenye masuala ya michezo kwa nyakati hizi.

Wale ambao wanaasili ya ugomvi kwenye mioyo yao kuanzia sasa waanze kufanya mazoezi ya kuutoa ugomvi kwenye akili zao na kuanza kujifunza kupenda amani itakaa ndani yao na hawatakuwa na ile hali ya zamani.

Mashabiki tuache kabisa kuziruhusu tofauti zetu za nyakati zilizopita, tuache kuwa na roho za visasi hazijengi kwa namna yoyote ile. Tanzania ni taifa letu na chaguo letu ni Timu ya Taifa ya Tanzania katika kuipa sapoti tofauti zote tuziweke kando.

Bado tuna safari ndefu kufikia mafaniko ambapo yamejificha lakini tusisahau kwamba mafanikio huja kwa kupenda kile ambacho tunakifanya. Tukiipenda timu yetu ya Tanzania na kuweka kando tofauti zetu kila kitu kitakuwa sawa.

Kwa upande wa wachezaji wasifikirie kuitwa timu ya taifa wamemaliza kazi hapana bado wana kazi nyingine ngumu ndani ya uwanja. Wasifikiri kwamba mashabiki wanapenda kutazama jezi mpya ambazo zimezinduliwa hilo halipo kwenye akili za mashabiki.

Kiujumla mashabiki wanahitaji kuona soka safi likipigwa ndani ya uwanja na ushindi ukipatikana ndani ya dakika 90. Ikiwa timu ipo nyumbani basi na icheze kwa kujiamini huku kila mchezaji akitimiza majukumu yake kwa umakini.

Rai yangu tujitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa Oktoba 11 kuipa sapoti timu yetu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars huku zile tofauti zetu zote tukiziweka kando jumlajumla.

 

 

1 COMMENTS:

  1. Ni kweli. Wamelipata walio na,tofauti ambazo hazina maana..pia ushindi ndy mhimu..

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic