CHRISTINA Mwagala, Ofisa Habari wa KMC amesema kuwa baada ya timu hiyo kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania hasira zao ni kwenye mchezo wao wa ligi dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Mchezo huo utachezwa Uwanja wa Uhuru, Oktoba 14 unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa timu zote zimetoka kupoteza pointi tatu kwenye mechi zao tatu zilizopita.
KMC Oktoba 5 ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania Uwanja wa Uhuru na Coastal Union ilifungwa mabao 3-0 dhidi ya Yanga, Oktoba 3.
Ofisa Habari wa KMC, Christina amesema kuwa makosa waliyoyafanya kwenye mechi zao mbili zilizopita wameyaona na watayafanyia kazi.
“Tulipoteza mchezo wetu wa kwanza uwanja wa nyumbani haina maana kwamba tutaendelea kupoteza hapana bado tuna mechi nyingi na tutaanza na Coastal Union Uwanja wa Uhuru Jumatano tunaamini tutafanya kweli.
"Mashabiki wasikate tamaa mapambano bado yanaendelea na KMC ina wachezahi wazuri wenye uwezo hivyo kwa sasa ni wakati wa kuendelea kupeana sapoti ili kupata matokeo chanya," amesema.
KMC ipo nafasi ya saba ikiwa imecheza mechi tano ina pointi 9 kibindoni inakutana na Coastal Union ambayo imecheza mechi tano na ina pointi nne ikiwa nafasi ya 15.
0 COMMENTS:
Post a Comment