LEO Jumapili pale Uwanja wa Mkapa jijini Dar, Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars itashuka dimbani kukipiga dhidi ya Timu ya Taifa ya Burundi, Intamba m’Urugamba, katika mchezo wa kirafiki uliopo kwenye Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Taifa Stars chini ya kocha mkuu, Etienne Ndayiragije, tayari imefuzu hatua ya makundi kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022 huku ikifuzu pia kushiriki michuano ya Chan itakayofanyika Januari mwakani.
Tangu kocha huyu achukue mikoba ya kuinoa Taifa Stars, amekuwa na mwenendo mzuri akirithi mikoba ya kocha aliyeipeleka Tanzania michuano ya AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39, Emmanuel Amunike raia wa Nigeria.
Ni imani yetu kuwa mchezo huu wa kirafiki utatumika kama sehemu ya maandalizi ya timu ya taifa ambayo Novemba, mwaka huu itakuwa na mechi dhidi ya Tunisia katika kufuzu Kombe la Dunia 2022 michuano itakayofanyika nchini Qatar, pamoja na michuano ya Chan kule nchini Cameroon.
Watanzania tujitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu yetu ya taifa ili itutoe kimasomaso kwenye kila hatua tunayopiga, wanajeshi wetu wako tayari kwa ajili ya kulipigania taifa, hivyo tuwaunge mkono.
Kwenye benchi la ufundi wapo makocha bora wakiongozwa na Ndayiragije raia wa Burundi, huku wasaidizi wake wakiwa ni wazawa, Selemani Matola pamoja na Juma Mgunda ambao kwa pamoja tangu waanze kuifundisha timu hiyo kumekuwa na matokeo mazuri tofauti na awali.
Wachezaji wanaounda kikosi chetu cha timu ya taifa wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa kule Uturuki na wengine wengi, tunaamini kwamba wanatambua namna Watanzania walivyo na kiu ya kuiona timu yao kila kukicha ikifanya vizuri bila ya kujali aina ya mechi tunayokwenda kucheza
Viingilio kwenye mchezo huo ni rafiki kwa watu wenye uchumi wa kati, hivyo tuoneshe uzalendo kwa kukata tiketi mapema na kuujaza Uwanja wa Mkapa kushuhudia wanajeshi wetu wakilipigania taifa.
Burundi ni timu ambayo uwezo wetu na wao haupishani sana, hivyo kuna kitu cha ziada kinatakiwa kufanywa ili kuhakikisha kuwa tunaibuka na ushindi.
Ukitazama rekodi ya michezo iliyopita tangu mwaka 1971, tumewafunga mara 13, wao wametufunga mara tano na sare tatu katika jumla ya mechi 21.kwa hivi karibuni Tanzania kupitia Ligi Kuu tumezidi kujizolea umaarufu kwenye mataifa jirani, hivyo tuzidishe hamasa, tujitokeze kwa wingi kwa Mkapa, wadau wa Temeke, Kinondoni, Ilala na hata wale wa mikoa jirani tujitokeze kwa wingi tuujaze uwanja.Kila kheri Taifa Stars katika mchezo wa leo, tunaamini mtafanya vizuri ndani ya dakika tisini pale kwa Mkapa.
0 COMMENTS:
Post a Comment