KILICHO mbele yetu kwa Taifa letu la Tanzania ni mchezo wa kitaifa wa kirafiki dhidi ya Burundi ambao upo kwenye kalenda ya FIFA. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Oktoba 11 Uwanja wa Mkapa. Uwanja wetu wa nyumbani ambao wakati mwingine umekuwa ukitoa majibu ambayo hayafurahishi. Kwa kuwa kwa sasa tayari wachezaji wameshaanza kujiweka sawa kujiwinda na mchezo huo wakati wao ni sasa kutimiza majukumu yao. Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania mnajukumu lingine mbele yenu kwa sasa ambalo linawahusu wenyewe tena bila kusahau ni kwa manufaa ya taifa kwa ujumla. Mnaingia vitani Jumapili kupambana na Burundi, sio kazi nyepesi ambayo ipo mbele yenu kwa sasa hasa ukizingatia kwamba mpira wa sasa ni ushindani na kila timu inatafuta ushindi. Nina amini kwamba mnatambua nini mnahitaji na mna kazi ya aina gani ambayo ipo mbele yenu kwa sasa hivyo ni muhimu kuungana kwa pamoja kupambana kwa ajli ya Taifa hicho ndicho kinatakiwa. Kazi ni kubwa na mnapaswa kujituma ndani ya uwanja kupata ushindi itakuwa furaha kwa mashabiki ambao watajitokeza kuwapa sapoti. Mna kazi ngumu ya kuwaaminisha watanzania kwamba hamjaitwa bahati mbaya kwenye kikosi cha timu ya taifa ambacho kinawakilisha Bendera ya Taifa kiujumla na jukumu ni zito kwa kweli. Kwa sasa akili zenu zinapaswa ziwe kwenye kupata matokeo mazuri. Kisha baada ya hapo furaha itakuja baadaye na mambo mengine ambayo huwa yanatokea yatatokea baadaye. Kikubwa kinachohitajika kwenye mpira ni maandalizi mazuri na sahihi hali itakayosaidia kupatikana kwa matokeo chanya uwanjani hakuna uchawi mwingine hapo. Hivyo wachezaji rekodi ambayo mliivunja mnapaswa mpambane iwe ya muendelezo kwa sasa kutokana na mazingira kuwahukumu endapo mtabweteka. Pia jambo jingine ambalo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatakiwa kufanya kwa sasa ni kuendeleza kutoa hamasa na elimu kwa mashabiki ambao wamekuwa na tabia za kupenda ugomvi. Hili ninaamini kwamba limeanza kupungua na ninafurahi kuona kwa sasa kwenye mechi nyingi zilizopita kwenye Ligi Kuu Bara wapo ambao wamekuwa wakishangilia kwa pamoja licha ya kuwa ni mashabiki wa timu tofauti. Nilipata bahati ya kushuhudia mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara ambao ulikuwa ni wa kuhitimisha raundi ya tano. Uwanja wa Uhuru kati ya KMC na Polisi Tanzania. Nilivutiwa na aina ya ushangiliaji wa mashabiki wa Polisi Tanzania pamoja na ule wa timu ya KMC. Licha ya KMC kupoteza dakika za lala salama bado mashabiki waliendelea kushangilia. Hata kwenye upande wa kukaa pia hakukuwa na bugudha yoyote kwa mashabiki kukaa. Kwenye viti vya mashabiki wa KMC walikuwepo pia mashabiki wa Polisi Tanzania. Ni furaha kuona kwamba tunaanza kujenga familia moja. Mana halisi ya mpira ni upendo na ushirikiano hivyo kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwa mashabiki kujitokeza Uwanja wa Mkapa kuipa sapoti timu yao. Hakuna kinachoshindikana ikiwa kila mmoja ataamua kufanya kwa kuzingatia wakati na kwa nidhamu. Mashabiki na wachezaji wote mna deni kwa sasa. Wachezaji mnapaswa mjitume na kuwa na uchu wa mafanikio kwenye mechi zote ambazo mtacheza kwa sasa uwanja wa Mkapa kupata matokeo. Hilo ndilo deni lenu kubwa la kwanza na la muhimu. Taifa linahitaji ushindi ninarudia tena ushindi kama haujanielewa nasisitiza tena ushindi ndio ambao Tanzania kwa sasa inasubiri. Kikubwa ili muweze kupata ushindi ni lazima mpambane kweli. Haina maana kwa kuwa matambua Tanzania inahitaji ushindi basi msijitume ndani ya uwanja hapana.Lazima mjitume. Mashabiki wote kwa sasa ni suala la kutambua kwamba ni wakati wa kuipa sapoti timu ya taifa bila kujali itikadi za timu zetu ambazo tunashabikia tukiwa nyumbani. Muda wa kujiwekea matabaka na makundi usiwepo tuwe kitu kimoja kwa kuwa taifa letu ni moja na asili yetu ni moja kuishi kwenye upendo muda wote. Hilo ni deni kwa masahabiki sasa. Hakuna haja ya kutengana katika hili kwa kuwa kushindwa kwa mmoja kutimiza wajibu wake kutaleta maumivu hapo baadaye. Tukiungana ni nafasi yetu kuweza kuongeza nguvu na ile amshaamsha kwa wachezaji kukumbuka kwamba wana deni nao kwa kwa tayari mashabiki mmeshalipa. Chuki za mashabiki hazijengi bali zinabomoa na kufanya mpira wetu ubaki palepale ulipo tubadilike na tupeane sapoti mwanzo mwisho kwa maendeleo yetu.
|
0 COMMENTS:
Post a Comment