LEO kikosi cha Azam FC kitakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu mbele ya Biashara United mchezo utakaochezwa Uwanja wa Karume, Mara.
Huu unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa kaimu kocha mkuu, Vivier Bahati kukaa kwenye benchi la ufundi baada ya Aristica Cioaba kufutwa kazi Novemba 26.
Akizungumza na Saleh Jembe, Bahati amesema kuwa maandalizi yapo sawa na wana amini kwamba watapata matokeo chanya mbele ya wapinzani wao Biashara United.
"Maandalizi yapo sawa hivyo imani yetu ni kuona kwamba timu inapata matokeo chanya ambayo yatatufanya turejee kwenye ramani.
"Kukosa matokeo kwenye mechi zetu zilizopita kwetu ni darasa hivyo mashabiki watupe sapoti tunaamini tutafanya vizuri," amesema.
Azam FC ilipoteza michezo miwili mfululizo ndani ya ligi kwa kufungwa mabao mawili ndani ya dakika 180 ikiwa ugenini na nyumbani.
Ilifungwa bao 1-0 na KMC Uwanja wa Uhuru na ilifungwa na Yanga bao 1-0 Uwanja wa Azam Complex.
Ikiwa imecheza mechi 12 imekusanya pointi 25 na kinara ni Yanga mwenye pointi 31 baada ya kucheza mechi 13.
0 COMMENTS:
Post a Comment