November 12, 2020

 


NOVEMBA 7, mwaka huu ilikuwa siku ndefu sana kwa wadau wa soka hapa nchini hii ni kutokana na ratiba ya mchezo mkali wa dabi ya Kariakoo, uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa 11:00 jioni.


Dabi hii inatajwa kuingia ndani ya tano bora za dabi maarufu barani Afrika kwa sasa, hii ni kutokana na idadi ya mashabiki ambao wamekuwa wakiifuatilia, huku wengine wakisafiri umbali mrefu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la kuja kuishuhudia.


Kwa hapa nyumbani Tanzania ni wazi inapotokea siku kukawa na mchezo baina ya Simba na Yanga, basi shughuli zote kuanzia za kisiasa hadi za kijamii husimama kwa siku nzima na kuacha tukio hilo kubwa lipite.


Hili linawezekana kutokana na ukweli kwamba hata wanasiasa nao wamekuwa wakigawanyika kwenye makundi haya makubwa mawili.


Kuna wakati hata familia hulazimika kutengana uwanjani, mke akiwa upande mmoja na mume akilazimika kukaa upande mwingine mfano mzuri wa hili ni kile kilichoonekana Jumamosi ndani ya familia ya staa wa muziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyelazimika kukaa upande wa mashabiki wenzake wa Simba akimuacha mama yake, Sanura Kassim ‘Mama Dangote’ akikaa upande wa mashabiki wa Yanga.


Mchezo huo tayari umepita, ukiisha kwa sare ya bao 1-1 na kuwaacha mashabiki wa timu hizo wakiendelea kutambiana huko kwenye vijiwe vya Kahawa na Pweza.


Baada ya kufunga ukurasa huo, nadhani huu ni wakati muafaka wa kuachana na itikadi zetu za Usimba na Uyanga na kugeukia majukumu ya utaifa wetu.


Hii ni kutokana na michezo ya ligi kusimama kwa muda ili kupisha ratiba ya kalenda ya michuano ya kimataifa.


Kwa sasa ni wakati wa kuweka pembeni masuala ya Yanga na Simba kwa kuwa yameshapita tuunganishe nguvu kuipa sapoti timu yetu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars pamoja na kuendelea na majukumu mengine.


Kesho Ijuma Novemba 13, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, nayo itaanza kibarua chake cha kusaka tiketi ya kushiriki AFCON dhidi ya timu ya Taifa ya Tunisia, nchini Tunisia na Novemba 17 itakuwa marudiano kwa Mkapa.


Ni wazi sisi wapenda michezo na Watanzania wote kiujumla tunapaswa kujitolea sapoti zetu za hali na mali ili kuweza kuwasapoti wanajeshi wetu hawa ili wapate kutuwakilisha vyema zaidi.

 

 Kila kitu kinawezekana kuanzia sasa kwa kuwa kwenye mchezo wa kwanza utakaochezwa kesho Novemba 13 ushindani utakuwa mkubwa lakini kuna unafuu kidogo kwa kuwa mashabiki hawataingia kutokana na zuio la Caf kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.


Lakini kwenye mchezo wa marudio utakaochezwa Uwanja wa Mkapa hapo mashabiki nusu wataruhusiwa kuingia hivyo ni muhimu kuanza kujipanga kwa wakati huu ili kuona kwamba timu inapata sapoti kwa kutoka kwa kila mmoja na kufuata utaratibu utakaowekwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic