November 9, 2020



UKIZUNGUMZIA mabondia wanaofanya vizuri kwenye ngumi za kulipwa nchini  basi huwezi kumshahau Saleh Mkalekwa  anayekipenda kipaji chake na kukitendea  haki  anapokuwa ndani ya ulingoni.

Mkalekwa mtoto wa Mbagala anatarajiwa kupanda ulingoni Novemba 28, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Next Door uliopo Masaki dhidi ya Ramadhani Shauri.

 

Bondia huyo anapanda ulingoni katika pambano ambalo limedhaminiwa na Gazeti la Spoti Xtra, +255 Global Radio, DSTV, Plus Tv, Kebby Hotel na kinywaji cha  Smart Gin.

Mkalekwa amefanya mahojiano maalumu na Spoti Xtra kuelekea katika pambano hilo ambapo amefunguka mambo mbalimbali  katika mchezo huo yakiwemo maisha yake.

Bondia huyo ameanza kwa kufunguka pambano lake la kwanza kucheza katika ngumi za kulipwa lilivyokuwa.

 

“Pambano langu lilikuwa zuri, nilipambana vizuri, suala la kulipwa hilo ni juu ya bondia siwezi nikaliongelea kwamba nililipwa kiasi gani.

Una familia?

“Ndiyo nina familia ya mke na watoto wa tatu, wakike wawili na wa kiume mmoja na wote naishi nao pamoja.

Ratiba yako ya mazoezi ikoje? 

“Muda wangu wa mazoezi huwa nafanya asubuhi na jioni, asubuhi naanza kutoka saa kumi na mbili kasoro mpaka saa mbili kasoro na kwa upande wa jioni naanza kutoka saa kumi na moja kasoro mpaka saa moja.

“Nafanya mazoezi ya viungo na kukimbia na pia nafanya mazoezi kutokana na mapambano  ambayo nacheza.

Unapenda chakula gani ?

 “Napenda sana kula vyakula vya asili yangu, kama ugali dona, dagaa, bamia, mboga za majani na matunda na hivi vyote napenda kula mchana.

Suala la ushirikina kwenye ngumi unazungumziaje?

“ Masuala ya ushirikina katika ngumi yapo hasa kwa watu wa Afrika, tunaamini masuala hayo lakini nachoamini katika mchezo ili ushinde mchawi wako ni mazoezi na hakuna kingine.

 “Ukifanya mazoezi na kuwa na nidhamu  mwishoni kutakuwa na matokeo mazuri ila siyo mambo ya ndumba.

 Umejipanga vipi kuelekea katika pambano lako dhidi ya Ramadhani Shauri?

“Kwanza namshukuru Mungu kuweza kufikia hapa nilipofikia, naendelea vizuri na mazoezi yangu, nimejipanga vilivyo kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki wangu wanaopenda  ngumi na watanzania kwa ujumla.

“Nawataka mashabiki wangu wakae mkao wa kupata burudani ya Mkalekwa, wajitokeze kwa wingi waone maajabu yangu,  wengi hawajanijua na kuniona maana nilikuwa napambana sana ngumi za nje kwa kipindi kirefu.

 “Mpinzani wangu Ramadhani Shauri ajipange vizuri maana nipo kivingine, muda mrefu alikuwa anakimbiakimbia leo amenihitaji sasa ajiandae vizuri nae tuonyeshane ubabe maana ngumi hazina mwenyewe.

“Kauli yangu kwa mashabiki nawaambia kwamba kuongea sana siyo ndiyo kupigana ila mikono ndiyo inaweza kuongea ulingoni na kila mtu atakusifu kwa neno lake na wengi wanatutengenezea jina katika ulingo.

“Baada ya pamabano langu la Novemba 28, mwaka huu kuisha natarajia kwenda nchini Nigeria kucheza pambano la ubingwa wa Afrika (WBF),” anasema Mkalekwa.   

Mbali ya pambano hilo, kutakuwa na mapambano  ya kimataifa kati ya bondia  Mtanzania kutoka Tanga, Salim Mtango atazichapa na bondia kutoka nchini Ufilipino, Eduardo Mancito ‘The Nightmare’ wakati Mtanzania , Idd Pialali yeye akitarajia kumvaa Arnel Tinampay kutoka Ufilipino.

 

Lakini mkali kutoka katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Selemani Kidunda atapanda ulingoni kugombania mkanda wa ubingwa wa PST dhidi ya mkongwe Said Mbelwa huku  Ramadhani Shauri  akimalizana na  Saleh Mkalekwa.

Wengine ni Shadrack Ignas  atayezichapa na Vicent Mbilinyi wakati Ismail Galiatano kutoka JWTZ akimaliza utata na Mustafa Doto wakati Adam Yusuph  wa Dar yeye atakuwa na kibarua kipevu dhidi ya Adam Kipenga kutoka jijini Tanga huku wanadada  Lulu Kayage atamaliza ngebe na   Stumai Muki huku mkongwe Japhet Kaseba akitarajia kupasuana na Imani Mapambano.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic