TANGA
imekuwa maarufu katika mchezo wa ngumi za kulipwa kupitia Hassan Mwakinyo
kutokana na rekodi anazoendelea kuweka katika mchezo huo.
Lakini wapo mabondia wengi wakali wanajua kazi
yao ndani ya ulingo isipokuwa hawajatoka tu, sasa huyu ni Adam Yusuph Chiga mmoja
kati ya mabondia matata sana wanaotokea Makorora jijini Tanga.
Kijana mmoja mpole sana lakini anaposimama
ndani ya ulingo anakuwa na roho ya kinyama kutokana na kushusha vyuma vya maana
kwa wapinzani wake.
Chiga
anatarajia kupanda ulingoni Novemba 28, mwaka huu kuzichapa dhidi ya Adam
Kipenga katika pambano litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Next Door Masaki jijini
Dar chini ya udhamini wa Gazeti la Spoti Xtra, +255 Global Radio, DSTV, Plus
TV, Clouds Media, Precision Air, Smart
Gin, Kebbys Hotel na Uhuru FM.
Championi limefanikiwa
kufika jijini Tanga na kumshuhudia bondia huyo akiendelea na maandalizi ya
pambano lake hilo chini ya kocha wake Zuber Abdulrahman ‘Mabele’ pamoja na
kuendelea na shughuli zake za bodaboda.
Chiga anasema kuwa: “Mimi ni mtoto wa tatu
katika familia ya watoto watatu ambao kuna wanawake wawili na wakiume mmoja
ambaye ndiyo mimi Adam.
“Katika
familia yetu peke yangu ndiyo nacheza ngumi yaani bondia lakini dada zangu wao
wanaendelea na shughuli zao nyengine.
“Naamini
ngumi zitanifikisha mbali kwa sababu nina kipaji cha mchezo huu halafu pia
naupenda lakini bado napata sapoti ya kutosha kutoka kwa watu wangu hasa wa
mtaa wa Kwa Njeka ambao natokea pia maskani zangu za Jerry Press na Johannesburg.
“Binafsi
nimejiandaa vizuri kwa sababu hakuna pambano dogo maana hata mpinzani wangu
naye amejiandaa hivyo sitegemei kuona pambano rahisi isipokuwa malengo yangu ni
kupata ushindi hilo ndiyo kubwa.
“Mbali ya
ubondia nafanya kazi ya kusafirisha watu kwa kutumia pikipiki yaani Bodaboda ndiyo
kazi kubwa ambayo naitegemea kuendeleza maisha.
“Unajua ngumi hatupigani kila siku ndiyo maana
nafanya kazi hiyo na ratiba yangu inaenda sawa kila siku kwa kuwa usaidizi wa
kutosha kutoka kwa watu wananiunga mkono.
“Nategemea ushindi katika pambano langu hilo
ndiyo jambo kubwa kwa sasa, nashukuru familia yangu nayo inaniunga mkono kwa
asilimia zote hivyo sitaki niwaangushe pale Next Door Masaki,” anasema Chiga.
Mama yake afunguka
Championi
halikuishia hapo kwani lilifanikiwa kuzungumza na mama mzazi wa bondia huyo, Saum Ramadhani
ambaye kwa upande wake amesema alivyogundua kipaji cha mtoto wake katika suala
zima la mchezo wa ngumi.
“Niligundua
kipaji chake wakati anaanza lakini hata ilipokuwa ikitokea amefanya kosa basi
ukitaka kumuadhibu ilikuwa shughuli pevu kwa sababu alikuwa na nguvu za mikono.
“Kiukweli hapo ndiyo nikajua kwamba anakipaji
na alipomaliza elimu yake ya sekondari ndiyo akaingia rasmi kwenye mchezo huu
wa ngumi.
“Nilichokifanya nikumuunga mkono na kumwambia aongeze bidii
katika mazoezi yake kwa sababu michezo sasa hivi ni ajira lakini pia wazazi
wengine wawaunge mkono vijana wao waliojiingiza kwenye michezo.
“Kitu
kikubwa ni kumuombea afanye vizuri katika pambano lake la Novemba 28, matumaini
yangu kwamba siku hiyo nitakuwepo kumuunga mkono,” anasema Saum.
Wengine
watakaopanda ulingoni ni Idd Pilali dhidi ya Arnel Tinampay kutoka Ufilipino,
Salim Mtango na Eduardo Mancito wa Ufilipino, Adam Yusuph dhidi ya Adam
Kipenga.
Wakati Seleman Kidunda atazichapa na Said
Mbelwa, Ismail Gali ya tano dhidi ya Mustafa Dotto, Ramadhan Shauri vs Saleh
Mkalekwa na Stumai Muki vs Lulu Kayage.
Pambano hilo
ambalo litakuwa kwa kiingilio cha Sh 20,000 mzunguko, Sh 50,000 kawaida na Sh
100,000 kwa VIP.
0 COMMENTS:
Post a Comment