MSHAMBULIAJI wa Simba, Mkongomani, Chris Mugalu, amerejesha matumaini kwenye kikosi cha timu hiyo katika kuelekea Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mkongomani huyo alikuwa nje ya uwanja kwa michezo mitatu akiuguza maumivu ya nyonga ambayo ni dhidi ya Tanzania Prisons, Ruvu Shooting na Mwadui FC.
Daktari mkuu wa timu hiyo, Yassin Gembe, amesema mshambuliaji huyo amepona kabisa na suala la kucheza Jumamosi dhidi ya Yanga lipo chini ya kocha mkuu, Sven Vandenbroeck.
Mugalu ametupia jumla ya mabao matatu ndani ya Simba ambayo imefunga mabao 21 baada ya kucheza mechi 9.
Gembe aliongeza kuwa, muda wote ambao Mugalu alikuwa nje akiuguza maumivu, alikuwa akifanya mazoezi binafsi chini ya uangalizi wa kocha wa viungo, Adel Zrane.
"Mugalu alipona maumivu yake muda mrefu na alikuwa akifanya mazoezi binafsi chini ya uangalizi wa kocha Adel kabla ya kuungana na wenzake ili kumuongezea fitinesi ya kutosha,” alisema Gembe.
Katika mchezo wa dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar, katika kuonesha kwamba amepona, Mugalu aliingia uwanjani dakika ya 62 kuchukua nafasi ya John Bocco.
0 COMMENTS:
Post a Comment