November 2, 2020

 


MWEZI Novemba umeingia na taratibu umeanza kwenda mbele kuelekea siku zake za kumalizika na kuja mwezi mwingine. Katika soka kwa mwezi huu ni muhimu zaidi kwa timu zetu ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa.

Timu hizo kwa hapa nyumbani ni Simba na Namungo, ambapo Simba watakuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Namungo ya Lindi wenyewe watapambana katika Kombe la Shirikisho.

Labda timu hizo zitakuwa zimesahau lini wataanza kuliwakilisha taifa katika michuano hiyo mikubwa kwa Afrika, lakini wanatakiwa kukumbuka mashindano ya mwaka huu yataanza Novemba 27, kwa maana bado wiki chache tu kuanza.

Ukiangalia mwendo wa wawakilishi wetu kwenye ligi hauridhishi sana kiasi kwamba inazua hofu pale ambapo watakapoanza kushiriki michuano hiyo ambayo inahusisha timu vigogo wa soka la bara hili.

Tunataka kuwakumbusha kuwa waanze kuangalia mwenendo wao na kubadilika mapema kabla ya mechi hizo kuanza kwa sababu hatutaki timu zetu ziwe shiriki bali wapambanaji.

Itapendeza zaidi mkianza maandalizi ya michuano hiyo kwa wakati huu japokuwa kuna mechi za ligi ambazo mnaendelea kucheza.

Kwa mwaka huu walau timu zetu zifanye jambo na zifike mbali baada ya msimu uliopita kuanguka mapema licha ya kuwa na wawakilishi wanne kwenye michuano hiyo.

Mwisho kabisa kumbukeni kufanya kwenu vizuri katika michuano hiyo nje ya kuwafungulia soko wachezaji wenu lakini pia inakuwa faida kwa nchi kurudisha nafasi yake ya kuingiza timu nne kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita.


Namungo FC ikiwa ni mara ya kwanza kuiwakilisha nchi kimataifa kuna kazi kubwa ya kufanya ndani ya Kombe la Shirikisho kwani ushindani wa huko sio sawa na ule ambao upo kwenye Ligi Kuu Bara.



Mnapaswa kuonyesha kwamba hamjafika huko kwa bahati mbaya bali mpo imara na mnaweza kufanya yote kwa umakini na kuwatoa kimasomaso Watanzania.


Kila kitu kinawezekana ikiwa mipango itaanza kupangwa kwa wakati huu ambao muda bado upo na inawezekana kufanya vizuri.


Hakuna Mtanzania ambaye atapenda kuona mambo yaliyotokea msimu uliopita kwa timu zote nne kuboronga mapema bali kinachotakiwa ni matokeo mazuri ndani ya uwanja.


Simba pia ambao ni mabingwa watetezi kazi yao ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huko wanakutana na muziki wenyewe wa wababe wenye uwezo.


Zile tanotano za zama zile pamoja na kuangukia pua mapema sio jambo zuri kwa mashabiki na taifa pia muda wa maandalizi ni sasa na kila mmoja afanye kazi yake kwa umakini.

 

1 COMMENTS:

  1. Hayawezi kuanza mwezi huo mpaka ligi ya mabingwa itakapimalizika Na imesimama baada ya wachezaji takribani 10 WA Raja Casablanca kuripotiwa kuwa Na covid 19.Ila team zinapaswa kujiandaa ngoma itakuwa mwakani

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic