November 28, 2020


 JAMBO moja ambalo kwa sasa linasubiriwa ni kuona namna wawakilishi wetu kwenye michuano ya kimataifa wanaweza kufanya vizuri kutokana na kuwa na kibarua kusaka ushindi.


Leo Namungo FC wanaanza kucheza saa 1:00 Uwanja wa Azam Complex kisha kesho Simba wao watakuwa na kazi ya kupambana nchini Nigeria wakiwa ugenini.

Namungo FC ambao ni wawakilishi kwenye Kombe la Shirikisho watakutana na Al Rabita ya Sudan Kusini wao tayari wameshatia timu kwenye ardhi ya Bongo wakiwa tayari kwa mchezo wa leo.

Kwa Namungo kwa kuwa watakuwa nyumbani mtihani wao wa kwanza ni kusaka ushindi jumlajumla kwa kuwa hakuna cha kupoteza hasa ukiwa nyumbani.

Sioni sababu ya Namungo kuanza kujilinda kwenye mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani bali wanatakiwa kuanza kupambana kusaka ushindi ndani ya dakika 30 za mwanzo kisha zile zitakazobaki watatakiwa kujilinda.

Kinachotakiwa ni ushindi hasa ukiwa nyumbani ili ukienda ugenini ukifanya mashambulizi ya kushtukiza huku ukilinda ushindi wako itatoa fursa ya timu kuendelea na kusonga mbele.

Ninaona wazi kwamba kwa namna ambavyo kikosi cha Namungo kilianza msimu huu bado hakijawa imara sana hasa kwenye upande wa ushambuliaji lakini haina maana kwamba hakina uwezo wa kushinda.

 

Kwa kuwa watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex ambao wamecheza mechi nyingi pale inawapa nafasi ya kuweza kupata ushindi mapema na kuandika rekodi mpya. Hawapaswi kutanguliza dharau bali wawaheshimu wapinzani.

 Watanzania wanahitaji matokeo chanya ili kuongeza furaha kwa kuwa hakuna ambaye anapenda kuona kwamba tunapoteza hasa kwenye mechi za kimataifa ambazo ni sehemu ya wachezaji pia kujitangaza.

Tukija kwa upande wa Simba hawa wanakwenda kukutana na kibarua kizito nchini Nigeria kwa kucheza na timu ambayo inaonekana kama haina rekodi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika lakini inapata matokeo.

Ninarudia tena kwa soka la Afrika ukiwa ugenini nafasi yako kushinda siku zote huwa inakuwa finyu ndio maana msimu ule ambapo Simba ilitinga hatua ya makundi mambo yalikuwa magumu kwa kupata matokeo yasiyo rafiki.

Kwa kuwa tayari wanauzoefu na mechi za ugenini za kimataifa mambo yalivyo wana kazi ya kufanya kwenye mechi ya kesho wakiwa nchini Nigeria.

 

Ikumbukwe kwamba msimu uliopita Simba haikufanya vizuri na iliishia hatua ya awali kwa kutolewa na UD Songo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini ambalo walilipata wapinzani wao.

Kwa msimu huu kazi itakuwa ngumu kwa Simba hasa ukizingatia kwamba wachezaji wengi wa Nigeria miili yao mikubwa na wanauwezo mkubwa ndani ya uwanja hiyo ni kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck.

Ni jambo jema kuwajua wapinzani kabla ya kukutana nao hivyo itatoa picha namna gani Simba ina kazi ya kusaka ushindi kwenye mchezo wa kesho.

Kwa namna ambavyo kikosi cha Simba kimeundwa na viungo wengi ambao uwezo wao ni kuchezea mpira ila pale mpira unapopotea hapo ndio tatizo huwa linaanzia ina kazi ya kuweka mabeki makini na viungo ambao watakuwa wapambanaji muda wote.

 

Kasi ya mabeki pia inabidi iongezeke hasa ukizingatia kwamba wachezaji wengi wa Nigeria spidi yao ni tofauti na ile ya wale wa Simba hapo kazi itakuwa nzito na hakuna wepesi kwa wawakilishi wetu wa Tanzania wakiwa ugenini.

Ninaamini kwamba ili ushindi upatikane kwa Simba ni lazima ifanye mashambulizi ya kushtukiza na kuweka ulinzi mkubwa ili wakipata sare iwe nafuu kwao kisha kazi ije kumaliziwa Uwanja wa Mkapa.

Kucheza na timu ambayo imeweza kuwa vinara ndani ya Nigeria yenye wazoefu kama Enyimba ambao walifungwa mabao 4-0 sasa hapo unadhani Simba ikiwadharau wapinzani wake nini kitatokea? 


Kila kitu kinawezekana na ushindi upo miguuni mwa wawakilishi wetu, imani yangu ni kwamba kila kitu kitakuwa sawa.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic