KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema kuwa ndani ya kikosi hicho kuna nyota wengi wanaoweza kuvaa kitambaa cha unahodha na kuwaongoza wenzake na sio lazima mara zote awe mchezaji mmoja au wawili pekee.
Hivi karibuni, kulizuka maswali mengi kuhusiana na ishu ya unahodha ndani ya kikosi cha Simba ambapo kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, aliyevaa kitambaa alikuwa Jonas Mkude licha ya uwepo wa nahodha mkuu, John Bocco na msaidizi wake, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Pia kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar, kitambaa hicho kilivaliwa na Bocco, alipotoka akamuachia Clatous Chama ambaye naye baadaye alimkabidhi Shomari Kapombe.Tshabalala ambaye katika mechi hizo zote alikuwepo uwanjani, licha ya kuwa yeye ndiye nahodha msaidizi, lakini hakupewa kitambaa avae hali iliyozua tetesi za kwamba kwa sasa ameenguliwa nafasi yake hiyo.
Akizungumza kuhusiana na sakata hilo, Sven amesema: “Kumekuwa na maswali mengi kuhusiana na ishu ya unahodha hasa baada ya kuwepo mabadiliko kidogo kwenye michezo miwili iliyopita, ambapo kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting tuliongozwa na Mkude huku michezo miwili iliyofuata Chama na Kapombe wakipata nafasi hiyo kwa vipindi tofauti.
“Kwangu sioni kama kuna shida kwa sababu wote tuna lengo moja la kuisaidia timu na kwa bahati nzuri ndani ya kikosi changu kuna wachezaji wengi ambao wanaweza kuongea na kuongoza wenzao uwanjani.
“Kama ilivyo kwa Mkude, Kapombe na Chama hivyo mchezaji yeyote anaweza kushika uongozi huo kuendana na upatikanaji wake uwanjani,” amesema Sven raia wa Ubelgiji.
Kwenye sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Yanga Uwanja wa Mkapa, nahodha alikuwa ni John Bocco na aliyeyusha dakika zote 90.
0 COMMENTS:
Post a Comment