BEKI mkongwe wa Simba, Shomari Kapombe, kamwe hatakubali kufanywa njia ya kupitia washambuliaji wa timu pinzani wa Yanga huku akiwataka watafute njia nyingine ya kupitia lakini siyo kwake.
Hiyo ni katika kuelekea pambano hilo la Dar es Salaam Dabi linalosubiriwa kwa hamu kubwa ambalo litapigwa leo Jumamosi Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mkongwe huyo aliyecheza Dar es Salaam Dabi nyingi, anatarajiwa kukutana na kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Mkongomani Tuisila Kisinda anayecheza winga wa kushoto namba 11.
Kapombe amesema kuwa mechi za dabi ndizo anazozitaka yeye, hivyo hana hofu ya pambano hilo na amejiandaa vema kupambana na mshambuliaji yeyote atakayekutana naye.
Kapombe amesema kuwa anafahamu umuhimu mkubwa wa pambano hilo ambalo ni lazima washinde ili wapunguze idadi ya pointi walizonazo wapinzani wao Yanga waliopo nafasi ya pili wakiwa na pointi 23, Azam FC 25 na Simba wenyewe 19.
Aliongeza kuwa hakuna kitakachoshindikana kwao kupata ushindi katika dabi hiyo kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya chini ya Kocha Mkuu, Mbelgiji Sven Vandenbroeck.
“Mechi za dabi ndiyo zangu ninazozitaka kucheza, kwani tangu nikiwa na Simba nimewahi kucheza dabi zote, hivyo nina uzoefu nazo.
“Binafsi nimejiandaa vema kukabiliana na mshambuliaji yeyote nitakayecheza naye nafasi moja, mimi kama beki nitatimiza majukumu yangu ya kulinda, kuokoa na kupunguza hatari zote golini kwetu.
“Hivyo sitakubali nipitike kirahisi na mshambuliaji yeyote kwani katika maisha yangu ya soka sijawahi kumuogopa mchezaji yeyote zaidi ninawaheshimu,” amesema Kapombe.
0 COMMENTS:
Post a Comment