November 29, 2020


 LEO Uwanja wa New Jos nchini Nigeria kutakuwa na kazi ya wanaume 22 ndani ya uwanja kusaka ushindi kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ambao ni wawakilishi wa kwa Tanzania watakuwa ugenini kupambana na Plateau United mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zote mbili kuhitaji kupata ushindi.

Kazi kubwa ni kusaka bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo bingwa anavuta mkwanja mnono ambao ni shilingi bilioni 5.7 jambo linalomaanisha kwamba vita yake leo itakuwa si ya mchezo.

Safari

Kikosi cha Simba kilikwea pipa Novemba 24 kikiwa na wachezaji 24 ambao watakuwa na kazi ya kusaka ushindi mbele ya Plateau United.

Safari yao ilianza Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kwa kupitia Ethiopia ambapo kilipumzika siku moja na kuibukia Abuja siku ya Jumatano, Novemba 25. Novemba 27 kikosi kilikwea pipa kutoka Abuja kuelekea mji wa Jos ambapo ndipo mchezo utachezwa majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Nigeria sawa na saa 12:00 jioni kwa hapa Tanzania.

Wachezaji waliopo

Aishi Manula, Ally Salim na Beno Kakolanya kwa upande wa makipa.

Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Clatous Chama, Francis Kahata, Hassan Dilunga, Bernard Morrison, Ibrahim Ajibu, Rarry Bwalya na Said Ndemla kwa upande wa viungo.

Mabeki ni Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Ibrahim Ame, Joash Onyango, Pascal Wawa na Kened Juma.

Washambuliaji ni John Bocco, Meddie Kagere, Miraj Athuman na Luis Miquissone.

Uwanja

Simba inakutana na Plateau United ambayo imeanzishwa mwaka 1975 inatumia Uwanja New Jos, huku Simba iliyoanzishwa mwaka 1936 ikiwa inatumia Uwanja wa Mkapa kwa mechi za nyumbani.

 

Uwanja wa New Jos una uwezo wa kuchukua jumla ya mashabiki 40,000 na kwenye mechi za nyumbani huwa inatumia jezi za rangi ya njano na ikiwa ugenini inatumia jezi za rangi ya njano mithili ya watani zao wa jadi Yanga

Mafanikio

Wapinzani wa Simba, Plateau United wamefanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya nchini Nigeria mara moja mwaka 2017 na wamepata zali la kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ligi yao kufutwa kutokana na janga la Virusi vya Corona.

Safu ya ushambuliaji

Wapinzani wa Simba kabla ya ligi kufutwa kutokana na janga la Virusi vya Corona wakiwa wamecheza mechi 25 walifunga jumla ya mabao 36. Kwa Bongo Simba imeonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji kwani kwa msimu wa 2019/20 ilifunga jumla mabao 78 lakini ilicheza jumla ya mechi 38 ikiwa ni tofauti ya mechi 13 hivyo ina kazi kubwa ya kufanya leo kuendeleza rekodi zake.

Ulinzi

Safu yao ya ulinzi ya Plateau United iliruhusu mabao 15 baada ya kucheza mechi 25 huku ile ya Simba ikiruhusu kufungwa mabao 21 bada ya kucheza mechi 38.

Ulinzi imekuwa ikionekana ni tatizo kubwa kwa Simba chini ya Joash Onyango na Pascal Wawa ambao wamekuwa wakipata tabu hasa wanapokutana na washambuliaji wenye kasi, hata kwa msimu huu wa 2020/21 ikiwa imecheza mechi 11 na imefungwa mabao matano jambo linalomaanisha kwamba Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck ana kazi ya kufanya mbele ya Wanigeria hawa.

 

Sven aliweka wazi kwamba wanaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kwa kuwa wachezaji wa timu pinzani ni wenye maumbo makubwa na uwezo mkubwa wa safu ya ushambuliaji.

“Tunawatambua wapinzani wetu ni timu imara na ina uwezo mkubwa hasa kwenye safu ya ushambuliaji pamoja na kuwa na wachezaji wenye maumbo makubwa tofauti na wachezaji wetu ila haitupi tabu.

“Malengo yetu tangu awali ni kupata ushindi kwenye mchezo wetu hivyo tunaamini tutafanya vizuri ili kufikia malengo yetu,” alisema.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic