November 11, 2020

 


KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze amesema kuwa kutokuwepo kwa nyota wake mtengeneza mipango namba moja kwa wageni Carlos Carlinhos ni miongoni mwa sabab iliyowafanya washindwe kusepa na ushindi jumlajumla kwenye Dar Dabi.


Yanga, Novemba 7 iligawana pointi mojamoja na Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa ambapo bao la kuongoza lilifungwa dakika ya 31 na Michael Sarpong kwa mkwaju wa penalti.


Bao la Simba la kuweka mzani sawa lilifungwa dakika ya 86 na beki, Joash Onyango ambaye alisababisha penalti dakika ya 28 baada ya kumchezea faulo, Tuisila Kisinda na mwamuzi Abdalah Mwinyimkuu kuamuru ipigwe penalti.


Kaze amesema kuwa waliweza kuwa bora kipindi cha kwanza na kipindi cha pili walizidiwa uwezo kwenye umiliki wa mpira jambo ambalo liliwapa nafasi wapinzani wao kuweka mzani sawa.


"Kipindi cha kwanza tuliweza kufanya umiliki mkubwa wa mpira lakini kipindi cha pili hali ilibadilika, ninaamini kwamba iwapo Carlinhos angekuwa mzima hasa kwa upande wa viungo kuna jambo lingetokea.


"Ulikuwa ni mchezo mzuri kwetu na wapinzani nao walikuwa imara, niliwaambia wachezaji kwamba kucheza na timu ambayo ipo kambini kwa muda mrefu zaidi ya msimu mmoja sio kitu chepesi.


"Lakini kwa walichokifanya ninawapongeza wanastahili pongezi tutafanya vizuri mechi zijazo," amesema.


Yanga ipo nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 10 kibindoni ina pointi 24 na vinara ni Azam FC ambao wana pointi 25 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi 20.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic