NYOTA wa kikosi cha Azam FC, Prince Dube leo anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania akitokea Afrika Kusini alikokwenda kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Dube mwenye mabao sita na pasi nne za mabao kati ya 19 ambayo yamefungwa na Azam FC iliyo nafasi ya pili na pointi 27 aliumia Novemba 25 kwenye mchezo dhidi ya Yanga.
Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ulikamilika kwa Azam FC kupoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema:" Baada ya kutibiwa kwa takrbani juma moja na nusu Prince Dube anatarajiwa kutua Bongo leo saa 5:45 usiku Desemba 13 akitokea nchini Afrika Kusini
"Dube aliumia mkono na ataondoka Afrika Kusini saa 8 mchana ili kurejea kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi ikiwa tayari ameshafanyiwa upasuaji ambao ulikwenda vizuri na ataanza mazoezi kwa ajili ya kujiweka sawa.
"Mwalimu wa viungo amesema kuwa japo ameumia mkono atapewa programu maalumu itakayomuweka kuwa fiti kwa kuwa bado hajarejea kwenye ubora wake.
"Ila kwa upande wa upasuaji ulikwenda vizuri hivyo tunaamini kwamba atarejea kwenye ubora wake hivi karibuni," amesema.
Kesho Desemba 14, Azam FC itakuwa na kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Namungo FC Uwanja wa Azam Complex.
0 COMMENTS:
Post a Comment