December 10, 2020

 


USHINDANI kwenye Ligi Kuu Bara ni mkubwa ambapo kila siku tunashuhudia rekodi mbalimbali zikiwekwa ndani ya uwanja baada ya dakika 90.

Jambo la msingi kwa wakati huu wa mzunguko wa kwanza ndani ya ligi ni kila timu kujipanga vizuri na kutumia nafasi ambazo wanazipata ndani ya uwanja kufanya vizuri.

Kwa sasa zipo ambazo zimeshajijengea ufalme wake kwenye kupaa matokeo mabovu zinapaswa zishtuke mapema kwana hali ikiwa hivyo mwisho wa ligi tutazungumza habari nyingine.

Zile ambazo mwendo wake ni mzuri zinapaswa pongezi na kuongeza juhudi hapo zilipo kwa kuongeza ushindani zaidi ili kuendelea kupata matokeo mazuri.

Hakuna timu ambayo inaingia ndani ya uwana ikiwa na hesabu za kupoteza mchezo zaidi ni kwamba kila timu inahitaji ushindi kufikia malengo ambayo wamejiwekea.

Kwenye vita ya kutafuta ushindi hapo ndipo kazi inabidi iwe kubwa kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kufanya vizuri katika kusaka matokeo chanya ndani ya dakika 90.

Kwa kupitia yale mapungufu ambayo benchi la ufundi limeyaona kwenye mechi zao zilizizopita hapo makosa yanatakiwa yafanyiwe kazi ili mechi zijazo makosa yapungue kabisa.

Ninapenda pia kuzikumbusha zile timu za Ligi Daraja la Kwanza kuendelea kupambania ndoto zao ili kufikia malengo ambayo yapo kwenye mipango kazi yao.

Nina amini kwamba huku kuna kiwanda kizuri cha kutengeneza wachezaji kwa ajili ya kesho hivyo ni muhimu kila mmoja akawekeza nguvu ndani ya uwanja na katika maandalizi pia.

Ili timu ipate matokeo jambo ni moja tu, maandalizi mazuri mambo mengine ni ya ziada kwani hakuna kinachowezekana kwenye maisha ya mpira ikiwa hakutakuwa na maandalizi mazuri.



Upo umuhimu wa kila mchezaji kutambua wajibu wake ndani ya uwanja na akiwa nje ya uwanja kwa kufanya mambo ambayo yanaleta matokeo mazuri kwake na timu.

Pia kuelekea kwenye dirisha dogo la usajili ni wakati muhimu kwa uongozi na timu zetu kuangalia namna gani zinaweza kuboresha vikosi vyao ili kuwa bora na imara.

Makosa ambayo yametokea kwenye mechi zilizopita pamoja na makosa ambayo yanaendelea kutokea ndani ya uwanja ni muhimu kutafutiwa dawa ili kuweza kupata matokeo mazuri kwenye mechi zijazo.

 Kuna timu ambazo zimepanda daraja msimu huu ikiwa ni pamoja na Ihefu, Dodoma Jiji hizi zimekuwa zikipata matokeo kwa namna ambavyo zimefanya usajili wao hivyo kupitia dirisha dogo zina jukumu la kuongeza nguvu pia.

Ikiwa zipo timu ambazo hazina uhitaji wa kufanya usajili kulingana na ripoti ya mwalimu hakuna haja ya kufanya hivyo bali jambo la msingi ni kutulia na kujipanga upya kwa ajili ya mzunguko wa pili.

Usajili uwe wa kufuata ripoti ya mwalimu na kila mchezaji inabidi ajue kwamba ikiwa anakwenda kuanza maisha mapya ana jukumu la kujipanga upya kukabiliana na changamoto mpya ambazo atakwenda kukutana nazo.

Muda ambao unahitaji utulivu kwa wachezaji ili kujua wapi wanakwenda kuanza maisha yao na muda wa kutulia kwa benchi la ufundi kujua kipi wanahitaji ndani ya timu.

Kwa wakati huu itapendeza kila timu ikawa na ripoti kamili ama ikajua ni aina gani ya mchezaji ambaye inamhitaji kuanza naye maisha kwenye kikosi cha timu zao.

Kwa mchezaji ambaye atapata timu mpya ana kazi la kuonyesha kile ambacho kimewavuta mabosi wake ndani ya kikosi ili awe bora zaidi na kufanya kazi yake kwa juhudi isiyokuwa ya kawaida kwenye kikosi ambacho atakwenda kuanza kufanya kazi.

Kwenye soka kila kitu kinawezekana na wale ambao bado wana mikataba yao na timu zao wanapaswa wafuate miiko ili kuepuka kuingia kwenye migogoro na mabosi zao.

Maisha ya mchezaji yanajengwa na kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja hivyo ikitokea akapata timu mpya ana jukumu la kulinda nidhamu na kufanya kazi kwa juhudi.

Ikiwa mchezaji atakuwa na nidhamu ndani ya uwanja ni rahisi kwake kufikia mafanikio ambayo anayahitaji. Ila kama itatokea hajali masuala ya nidhamu nirahisi kushuhudia anguko.

Hivyo ni jukumu la kila mchezaji kutazama namna bora ambayo itamfanya aweze kupata namba kule ambako anakwenda kuanza maisha mapya ndani ya soka.

Kazi ni moja kwa wachezaji wa Ligi Daraja la Kwanza na wale wa Ligi Kuu Bara kuhakikisha kwamba wanalinda uwezo wao na kutumia vipaji walivyo navyo kwa faida.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic