“UNAPOKUWA mchezaji malengo yako makubwa ni kucheza na kuonyesha uwezo wako, kama unakosa nafasi sehemu moja basi sio vibaya kwa kushirikiana na viongozi wako ukatafuta eneo jingine ambalo unaweza kucheza,” anaanza kueleza Straika matata wa kikosi cha klabu ya Simba Charles Ilanfya.
Ilanfya alijiunga na Simba akitokea kikosi cha KMC mwezi Agosti mwaka jana, lakini amekuwa na wakati mgumu msimu huu ambapo amecheza mchezo mmoja pekee wa kimashindano.
Ilanfya amepiga stori nasi na kufungukia mambo mengi kuhusu safari yake ya miezi sita tangu ajiunge na kikosi cha klabu ya Simba kama ifuatavyo;
Ligi iko kwenye mapumziko kaka, mipango yako imekaaje?
“Kwa sasa naendelea tu na mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha
nauweka mwili wangu katika hali ya utayari wa kupambana ili pale ligi
itakaporejea tena niwe fiti,”
Hujacheza michezo mingi mzunguko wa kwanza nini tatizo?
“Ishu kubwa ni ushindani wa namba kwenye kikosi, mimi siyo
mchezaji pekee ambaye sikucheza wapo na wengine na hiyo ni kutokana na ukweli
kwamba Simba ina kikosi kipana na mpira ni mchezo wa namba hivyo hatuwezi
kucheza wote.
Kutopata nafasi ya kucheza kumekuathiri kwa kiasi gani?
“Kwa mchezaji ni jambo la hatari sana kama hupati nafasi ya
kucheza mara kwa mara kwa kuwa hili hupelekea athari kwenye kiwango chako.
“Hivyo kwa kiwango fulani kutocheza kumeathiri hali yangu ya
kujiamini na kuharibu takwimu zangu.
Unahisi kocha Sven alishindwa kukuamini?
“Hapana, aliniamini na ndiyo maana alihitaji nisajiliwe Simba
ila changamoto ya kukosa kucheza ni kawaida kwa mchezaji mpya.
“Naamini kama angeendelea kuwepo kuna wakati ningepata nafasi
ya kucheza, kwa kuwa alikuwa akinisaidia sana kukuza uwezo wangu wa kujiamini.
Baada ya kuondoka kwa Sven umejipangaje?
“Kama mchezaji napambana kila siku kuonyesha uwezo sio tu kwa
kuwa kocha flani yupo au hayupo, hivyo najitahidi mazoezini ili kuhakikisha
naonyesha kiwango kizuri ili kumshawishi kocha yoyote anipe nafasi.
Unauzungumziaje ushindani wa namba Simba?
“Simba ni klabu kubwa na miongoni mwa sifa ya klabu yoyote
kubwa ni kuwepo kwa ushindani wa namba, hivyo sio jambo la kushangaa sana cha
muhimu kama mchezaji ni kujitahidi kuonyesha uwezo wako ili uweze kupata
nafasi.
“Na hicho ndicho ambacho mimi pamoja na wachezaji wenzangu
wote tunakifanya kwenye viwanja vya mazoezi ili kumshawishi kocha akupe nafasi
kwenye kikosi cha kwanza.
Hukuwahi kufikiria kutolewa kwa mkopo?
“Nimewahi kufikiria hivyo kwa kuwa kwa mchezaji ishu ya
kwanza na muhimu kabisa ni suala la kiuhakikisha unatunza kiwango chako kwa
kupata nafasi ya kucheza.
Coastal walikuhitaji kwa mkopo dirisha dogo nini kilienda
kushoto?
“Kila kitu kipo sawa mbona, utaniona tu sehemu nyingine
nafanya kazi.
Kwa mzunguko huu wa pili au?
“Yah, kuanzia mzunguko huu wa pili natarajia kufanya kazi katika kikosi cha KMC,"
Ni magumu gani umeyapitia ukiwa na Simba?
“Hakuna magumu yoyote niliyoyapitia zaidi ya kukosa nafasi ya
kucheza basi lakini kila kitu kilikuwa sawa.
Rafiki yako mkubwa Morrison naye hali tete, unadhani tatizo
liko wapi?
“Morrison kweli ni rafiki yangu mkubwa lakini siwezi
kumuongelea nachokijua mimi alikuwa anakosa nafasi ya kucheza kwa kuwa alikuwa
anaumwa lakini akiwa sawa najua atafanya vizuri.”
Unadhani Simba wanalazimika kusajili Straika mwingine kama
ilivyo mpango wao?
“Hapo siwezi kusema chochote kwa kuwa ni mambo ya uongozi,
wao kwa kushirikiana na benchi la ufundi ndiyo wanajua mapungufu ya kikosi na
kwanini wanafanya usajili wa mshambuliaji mwingine.
Unaionaje ligi ya msimu huu?
“Ligi ni bora na ngumu kwa kuwa kila timu inaonekana
kujiandaa vya kutosha, unaweza ukajiridhisha na hilo hata kwa kuangalia tofauti
ndogo za pointi zilizopo kati ya timu moja na nyingine kwenye msimamo.
“Katika hali kama hii ni muhimu kwa kila timu ikajitahidi kuhakikisha
inachanga karata zake vizuri kwenye kila mchezo.
Malengo yako msimu huu ni yapi?
“Malengo ya kila mchezaji ni kufanya vizuri na kuona anakuza
kiwango chake kila siku, msimu uliopita nikiwa na kikosi cha KMC nilifunga
mabao sita hivyo natamani kuona nakwenda mbele zaidi ya hapo msimu huu.
Tukio gani limewahi kukufurahisha zaidi?
“Kumbukumbu ya furaha niliyonayo kwenye maisha yangu ya soka
ni kufanikiwa kuzifunga Simba na Yanga nikiwa na KMC msimu uliopita, unajua hii
ni ndoto ya wachezaji wengi hasa sisi vijana.
Umepata mafanikio gani mpaka sasa kupitia soka?
“Ni vigumu kuanisha ni vitu gani nimefanikiwa kuvipata
kupitia soka, lakini nakiri soka limenisaidia kubadilisha hali ya maisha yangu
kwa mfano, kwa sasa naweza kujihudumia na kuhudumia familia yangu pia.
HONGERA DOGO, UMUVUNA MKWANJA SAFI INGAWA ULIKUWA BENCHI SIO MBAYA ILA UNAPASWA KUONGEZA KASI HATA HUKO UENDAKO
ReplyDeleteSubiri walizokupa Simba ziishe ndipo utajua ,maana ukiangalia pesa za msimu mmoja kuliko kipaji chako.
ReplyDelete