UONGOZI wa Namungo FC umesema kuwa una imani ya kufanya vizuri ndani ya Ligi Kuu Bara kwa kuwa wachezaji wamepata muunganiko kupitia Kombe la Mapinduzi.
Namungo inanolewa na Kocha Mkuu, Hemed Morroco imeshiriki kwa mara ya kwanza Kombe la Mapinduzi mwaka 2021 na ikaishia hatua ya nusu fainali.
Ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Simba huku nyota wao Erick Kwizera na Stephen Sey wakionyesha uwezo wa kazi ndani ya dakika 90 Uwanja wa Amaan.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Namungo FC, Kidamba Namlia amesema kuwa kila kitu kipo sawa na wanaamini watafanya vizuri kwenye mashindano yajayo pamoja na Ligi Kuu Bara.
"Tumekuwa kwenye hesabu kubwa za kufanya vizuri ndani ya Ligi Kuu Bara pamoja na mashindano ya kimataifa ambayo tunashiriki.
"Imekuwa ni kawaida kwa wengi kufikiri kwamba hatuna uwezo, hatuna wachezaji wa ushindani ila taratibu wanaanza kutuelewa kwa kuwa wanaona kazi tunaifanya kwa vitendo.
"Kikubwa ambacho kipo kwa sasa ni kuona kwamba namna gani tunaweza kuwa kwenye ule ubora ambao umeanza kuonekana, mashabiki wazidi kutupa sapoti tunaamini kwamba tutafanya vizuri," amesema Kidamba.
Kwenye Ligi Kuu Bara, Namungo FC ipo nafasi ya 15 ikiwa imecheza jumla ya mechi 14 imekusanya pointi 18.
0 COMMENTS:
Post a Comment