KWANZA nianze kwa kuwapongeza Simba kwa mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia michuano ya Simba Super Cup, ambayo ilianza kutimua vumbi kuanzia Jumatano iliyopita.
Michuano hiyo iliyofikia
kilele siku ya Jumapili ilishirikisha timu tatu za TP Mazembe ya Congo, Al
Hilal ya Sudani na wenyeji klabu ya soka ya Simba iliandaliwa rasmi kama sehemu
ya maandalizi ya timu hizo kujiandaa na michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya
Mabingwa barani Afrika.
Naamini michuano hiyo
imekuwa na tija kubwa kwa timu shiriki hasa katika kipindi hiki ambacho bado
maambukizi ya virusi vya Corona yamekuwa hatari maeneo mbalimbali duniani kiasi
cha kusababisha hata baadhi ya ligi kusitishwa.
Kutokana na changamoto hiyo
ya ligi nyingi kusimama kwa muda mrefu, wachezaji wanaocheza kwenye ligi husika
wamekuwa wakikumbana na tatizo kubwa la kukosa utimamu wa mwili ‘Match Fitness’
hivyo kuhatarisha utendaji kazi wao viwanjani.
Hivyo naamini hili haliwezi
kuwa tatizo tena kwa upande wa klabu ya Simba, kwa kuwa wao wamepata muda
mwingi wa kucheza kwa kulinganisha na wapinzani waliopangwa nao.
Lakini pia Simba wamenufaika
sana na ubora wa timu walizokutana nazo, kwa kuwa walialika timu ambazo
zinawiana kwa kiasi kikubwa na zile ambazo wamepangwa nazo katika hatua ya
makundi.
Simba ikiwa katika kundi A
pamoja na timu za Al Merrikh ya Sudani, AS Vita ya DR Congo na bingwa mtetezi
wa michuano hiyo klabu ya Al Ahly kutokea nchini Misri.
Hivyo ni wazi kuwa Simba
imepata kipimo na majaribio sahihi ya mitihani ambayo watakwenda kukutana nayo
kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kitu kingine nilichokipenda
kutoka Simba hasa katika kampeni yao ya kuhitaji kutinga hatua ya nusu fainali
ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni usajili walioufanya kwa lengo la kukiongezea
nguvu kikosi chao.
Limekuwa jambo la
kupongezwa kuona Simba ikitilia maanani na kufuata ushauri wa kocha wao
aliyepita, Sven Vandenbroeck ambaye alionya uwezekano wa baadhi ya timu kutumia
hujuma ya janga la Corona kudhibiti baadhi ya wachezaji muhimu wa vikosi vya
wapinzani.
Hivyo wamefanya hivyo ili
kuhakikisha wanakuwa na kikosi kipana na ndicho ambacho wamekifanya.
Licha ya maandalizi hayo
mazuri na ya kupongezwa, kwa upande wangu nadhani Simba bado wana vitu vingi
vya kufanya kuelekea michezo hiyo na hawapaswi kubweteka kwa kudhani watakutana
na ushindani rahisi.
Kwa kuanzia wakumbuke kuwa
ratiba ya michezo hiyo haipo mbali bali ni tarehe 12 tu ya mwezi huu wa
Februari, na ikumbukwe bado wana vibarua vya michezo yao ya viporo.
Nadhani wakati huu mtihani
ni mkubwa kwa kocha wa Simba Didier Gomes Da Rosa ambaye Wanasimba na wadau wa
soka Tanzania wanatamani kuona ni nini atakifanya ili Simba ifuzu hatua ya robo
fainali na hatimaye nusu fainali pamoja na kurejea tena kileleni mwa msimamo.
Uchambuzi wa Edibily
Lunyamila kupitia gazeti la Championi Jumatatu
ndiyo maana UONGOZI WAKAONGEZA NGUVU KATIKA KIKOSI, INA MAANA HAKUNA KUBWETEKA
ReplyDelete