February 15, 2021






Na Saleh Ally

WAKATI mechi kati ya Simba na AS Vita nilitaka kuwe na utulivu sana ili niweze kuangalia mambo kadhaa ya msingi na kubwa kwangu lilikuwa ni je, Simba walijifunza jambo kutokana na kile kipigo cha mabao 5-0 jijini Kinshasa miaka mitatu tu iliyopita.


Hofu kubwa kwangu, kwamba hata kama Simba walijifunza, nakumbuka walikuwa chini ya kocha Mfaransa, Patrick Aussems, baada ya hapo wakawa na Mbelgiji, Sven Vandenbroeck na mwisho wamerejea Kinshasa wakiwa na kocha mwingine Mfaransa, Didier Gomes, huyu ni mpya.



Kwamba wataweza, ingawa ni kwamba wachezaji wengi walikuwa ni hawahawa na hata kipa Aishi Manula ni yuleyule. AS Vita, tayari nilikuwa na taarifa haijapoteza mchezo takriban mwaka mzima. Kwangu soka ni burudani na kazi, nikasema nitajifunza huku nikiburudika kama ilivyo ada.



Ukaguzi wangu wa kwanza, ulianzia katika kikosi. Nikaona ni wachezaji wanne tu waliokuwa wamepata nafasi ya kuanza, kipa, mabeki wawili wa pembeni pamoja na kiungo mkabaji mmoja, si haba.


Baada ya mechi kuanza, nikaanza kuangalia namna ambavyo Simba walijipanga na kufanya mambo yaende. Nakumbuka katika mabao matano waliyofungwa, nakumbuka mipira mitatu ya adhabu na kona ndiyo iliwamaliza na wachezaji wa Simba hawakuwa wakiruka juu, wakafungwa mabao mepesi sana.


Katika mechi hiyo ya juzi, mambo yakawa tofauti na hakukuwa na nafasi ya mchezaji hata mmoja wa AS Vita kuruka peke yake. Kila adhabu na kona iliyoelekezwa kwa Simba, pale langoni ilikuwa hakuna kulala. Wazi nikajua Simba hili walilifanyia kazi na Gomes alishajua njia sahihi ya kupambana nalo.

 

Aina ya kupanga mashambulizi, Simba inajulikana. Aina ya ukabaki wa nguvu na utibuzi wa mashambulizi ikaonekana Simba kweli wamejipanga na binafsi nikasema kwa mwendo huu wanaweza wakaondoka hata na pointi moja badala ya kuamini wangefungwa mabao machache angalau mawili. Lakini mwisho, Simba wakaonyesha kweli walijifunza na sasa wamejipanga kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.


Kwa namna Simba walivyocheza, hakuna ubishi tena ni timu kubwa Afrika.  Hawakuwa wakiweweseka wala hofu ya kufungwa na badala yake walipambana kuzuia kuruhusu bao lakini wakatengeneza nafasi.



Hawakuonekana kama wako ugenini licha ya nidhamu kubwa waliyokuwa nayo kiulinzi na kimashambulizi. Walionyesha ni timu ya kiwango cha Afrika. Jambo ambalo ni gumu kuonekana kwa kuwa Watanzania tunapenda kujidharau.


Inawezekana kabisa kwa aina ya uchezaji wa Simba katika mechi hiyo na kama itaendelea hivyo katika mechi zijazo, basi wanakwenda kuwa gumzo barani Afrika. Kikubwa ni lazima waendeleze walichokianzisha.


Simba ni kubwa si kwa maneno tena na hasa unapozungumzia michuano hii mikubwa ya Afrika kwa ngazi ya klabu. Bila shaka hata Al Ahly sasa watakuja Dar es Salaam kwa tahadhari kubwa sana wakijua Simba si timu ya utaniutani tena.


Haina maana Simba haitakosea, au haitafungwa maana vigogo kama kina Ahly pia hufungwa na timu mbalimbali za Afrika. Simba walipofikia, Watanzania wanapaswa kujivunia na hakuna ubishi anayetaka kukua au kubadilika, Simba wanaweza kuwa mfano mzuri. Hapa ondoa mambo ya ushabiki, badala yake angalia au ujali mpira.



Jambo la kwanza, kwa misimu minne sasa, wameendelea kubaki na wachezaji walewale kwa asilimia 70. Wamekuwa makini katika uongezaji wa wachezaji wapya na sasa wanakwenda katika ile ndoto yao ya kuwa kigogo wa Afrika.


Tukubali, Simba wamepita hatua. Kama uko Tanzania na ukataka kuwabeza ni kujipiga vita mwenyewe. Utakuwa hautumii haki yako ya kujifunza kupitia chako au cha nyumbani kwenu, hapa nazungumzia kwa Watanzania. Hivyo, angalia hatua wanazopiga na unaweza kujifunza jambo likawa msaada katika kikosi chako.


Walichokifanya Simba kuifunga AS Vita pale Kinshasa, wametengeneza rekodi nyingine ambayo itadumu kwa muda mwingi, huenda wengine itakuwa vigumu kuwaelewa na hasa mwanzoni.


Lazima Simba wamejifunza kupitia misukosuko ya kufungwa tano mara mbili yaani Kinshasa na Ahly lakini leo, wameonyesha kuna mabadiliko yenye mafanikio, usikae nao mbali ili unyakue mambo.


 


5 COMMENTS:

  1. Basi tuibeze Simba na tuwasifu wale waliofungwa mara mbili mfululizo na timu za michangani wanaokabiliwa na adhabu ya kutosajili wachezaji kwa misimu mitatu kutokana na kutowalipa ajira za waliowafanyidha kazi

    ReplyDelete
  2. Watanzania sisi ni watu wa ajabu au wajinga kama si kosei kusema hivyo tafadhali.Hata Diamond tulimbeza na kumuona si chochote si lolote na mpaka hivi sasa tunavyozungumza bado kuna watanzania hawaoni kitu kwa Diamond.Lakini cha ajabu Diamond huyuhuyu angekuwa mkenya basi ungeona jinsi watanzania tunavyompamba.Watanzania tuna kasumba na ujinga wa kujidharau na ukikidharau cha kwako huwa unajidharau wewe mwenyewe utake usitake pengine bila ya kujua.Kwa bahati mbaya sana kasumba hizi za watanzania za kujibeza wao wenyewe kabla hata ya kubezwa na mtu wa nje zimewajaa hata wanasiasa wetu pia ambao wengi wao hutumia nguvu za ajabu kupinga kila kitu kizuri cha maendeleo kinachofanyika Tanzania kisa tu kwakuwa kitu hicho kinafanywa na mtanzania? Kwa mfano utaona mtanzania anaisifia nchi inayotutengenezea mazingira ya kuwa wakopaji kila siku na kumbeza mtanzania anaepambana kuondokana na kuwa nchi ya kukopa kila siku.
    Mfano kwa mtu mwenye akili timamu vipi utakwenda kuusifia uchaguzi wa Uganda na kuubeza ule wa Tanzania? Na kwa mtu mwenye akili timamu vipi utakwenda kuisifia Kenya na mfumo wake wa kisiasa kuwa wa kidemokrasia zidi,nchi ambayo ukabila na utabaka umekithiri,Ufisadi na unyanyasaji kwa raia ni kitu cha kawaida kabisa. Sina lengo la kuzungumzia siasa bali huu ndio ukweli halisi kwakuwa huwezi kuitenganisha Kenya na Tanzania ni kama nchi moja ila wenzetu hutukuza vya kwao hata kama vina makando kando na ndio wakati mwengine wanaonekana wapo juu kuliko sisi kupitia mazuri ya Tanzania au ya watanzania kwakuwa sisi wenyewe watanzania tumeshindwa au tumeacha kuyabeba yale yetu mazuri na kujitangaza nayo Duniani yakatubeba.Mfano kuna wale wanaosema simba kaifunga Es Vita kwa sababu Vita hiii ni nyepesi? Ati wachezaji kadhaa wazuri wa wakati ule wameondoka pale vita ndio maana vita imepoteza makali? Tena wanaozungumza hivyo sio watanzania wa vichochoroni ni watanzania wanaoishi kwa kazi za kuwahabarisha watanzania kuhusu habari za michezo.Wakati wanaigeria walipoiona simba ikicheza kule kwao bila ya kujali korona au Covid 19? Wanaigeria walitaka kujua kama kweli hii simba ni timu ya Tanzania? Na walipothibitishiwa kweli ni timu ya Tanzania walishtuka mno kwa kiwango walichikiona kule Nigeria na kuwatabiria makubwa. Platinum fc ni timu ngumu kweli kweli sio nchezo kwenye rekodi zao za miaka hii ya karibuni ila simba aliwafanya kuwa timu ya kawaida sana ila tunasubiri simba kufungwa mchezo mmoja tuanze kusema unaona tulikwambieni simba ni timu ya kawaida..whata Shame?.Kuondoka kwa wachezaji kadhaa wa ES Vita sio sababu ya kuwaondolea ubora wao na ndio maana unasikia hata mazembe ya pale pale kwao wameshindwa kuwafunga vita msimu huu.wakati vyombo vya habari vya michezo vya Africa vikishangazwa na kusifia ubora wa simba waliouonesha hadi Caf kurusha jumbe maalum kwenye kurasa zao jinsi kiwango cha simba kilivyowakosha sisi watanzania tunahangaika kutafuta jinsi gani tunaweza kupata sababu ya kuonesha kuwa simba haistahiki kupewa credit kwa kuifunga vita kwakuwa eti vita ilikuwa nyepesi? Alieturoga ni nani au ni roho mbaya tu? Ni msifu tu Salehe jembe kwa kuwa mweledi mno kwenye soka nikiri nilishindwa kumuelewa na kumkubali huko nyuma.Ila ni miongoni mwa waandishi wazalendo kwa vitendo inapokuja Tanzania kwenye masuala ya michezo hasa kwa vilabu vyetu hasa vijana wetu nakusudia wachezaji wetu wa kitanzania naona huwa anawajali kama ndugu wa damu kabisa kuta wafanikiwe,big up Jembe..keep it up.

    ReplyDelete
  3. πŸ‘πŸ‘πŸ‘†πŸ‘†

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic