TARATIBU zile ndoto ambazo ulikuwa umeziandika kwenye kile kitabu cha kumbukumbu zinazidi kuyeyuka kwa kuwa muda hausubiri na mapambano lazima yaendelee.
Ipo hivyo pia kwa wale wachezaji ambao kazi yao ni kusaka
ushindi ndani ya uwanja muda wote ili timu yao ipate pointi tatu.
Kuanzia Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu Bara huku kwa sasa vita
inayokwenda kuanza ni ya mzunguko wa pili ambao ni muda wa kukamilisha hesabu.
Wapo wachezaji pamoja na benchi la ufundi ambalo kwa mzunguko wa
kwanza walikuwa na ndoto za kumaliza wakiwa ndani ya 10 bora ila mipango
iligoma wakaishia chini ya nafasi ambazo walikuwa wakizipigia hesabu.
Ukitazama kwa haraka kwa sasa kuna timu nne chini ambazo
zimeanza kupoteza matumaini ya kufanya vizuri kutokana na kasi yao kuwa ya
kusuasua.
Itazame Ihefu FC ambayo imekuwa ikipambana kusaka ushindi ila
bado ipo nafasi ya 18 inakaribiana na Mbeya City iliyo nafasi ya 17 huku Mwadui
ikiwa nafasi ya 16.
Namungo licha ya kuwa na viporo viwili bado imekuwa kwenye kasi ambayo
hairidhishi kwani ipo nafasi ya 12 na kibindoni ina pointi zake 21.
Kazi kubwa kwa Kocha Mkuu wa Namungo, Hemed Morroco ni kusaka
ushindi kwenye mechi zake zote na asisahau kwamba ana kibarua kwenye mechi za
kimataifa.
Namungo inawakilisha nchi kwenye Kombe la Kimataifa katika Kombe
la Shirikisho na inapaswa ifanye vizuri huko pia hivyo sio kazi rahisi kuweza
kufikia mafanikio ambayo wanayahitaji ikiwa watashindwa kujipanga.
Achana na hao kuna zile mbili ambazo ni JKT Tanzania ipo nafasi
ya 13 na Coastal Union ipo nafasi ya 14, hili eneo pia sio salama yanaweza
kuwakuta yale ya Mbao FC ambayo ilishushwa daraja na Ihefu.
Nafasi ya 13 na 14 ikiwa watasalia hapo mpaka mzunguko wa pili
utakapokamilika inamaanisha kwamba wana kazi ya kucheza play off na timu kutoka
Ligi Daraja la Kwanza hivyo wakizubaa lolote linaweza kutokea.
Kikubwa ambacho kipo kwa sasa wachezaji wengi ambao timu zao
zipo nje ya 10 bora wanakutana na ushindani mkubwa na makosa yao yanakuwa ni ya
kujirudiarudia kushindwa kuwa makini.
Hili limekuwa likisemwa mara kwa mara na Kocha Mkuu wa Coastal
Union, Juma Mgunda ambaye alikuwa anasema kwamba wachezaji wake wanarudia
makosa jambo ambalo linaigharimu timu yake.
Ninapenda kuzikumbusha timu hizi kwamba ikiwa zitajisahau kwenye
mzunguko wa pili kupambana ndani ya uwanja kusaka matokeo chanya kuna suala la
kushuka daraja.
Ipo wazi kwamba ni lazima timu nne zishuke daraja na mbili
kucheza play off. Kwa zitakazoshuka inapaswa zijipange kwa kuwa huko kuna timu
zilishuka bado zinapambana kurejea ndani ya ligi.
0 COMMENTS:
Post a Comment