KUNA mambo mengi ya kupima ili kujua ulichonacho kina uzito au ukubwa upi. Wakati mwingine hauhitaji kukibeba kitu kujua ukubwa wake lakini utalazimika kukiinua kujua uzito wake.
Huu ni mzunguko wa pili, kipindi ambacho ni sahihi kujua kiwango cha ubora wa kila timu na huu ndio wakati yale makundi matatu hutengenezwa.
Aghalabu kuona makundi hayo matatu yanatengenezwa katika mzunguko wa kwanza. Kundi la kwanza ni la timu zinazoteremka daraja, hizi zitabaki kupambana kuepuka kuteremka daraja na katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, haitakuwa sahihi kuzitabiri hata kama ziko mkiani.
Kundi la pili, ni zile zilizokuwa na nafasi kubwa ya kubaki, nazo hugawanyika kundi A na B. A ni zile zenye uhakika na huwa ndio kundi la kwanza na zile ambazo zinabidi zipambane hasa ili kubaki.
Kundi la kwanza ni zile zenye nafasi ya ubingwa na kuanzia mzunguko wa pili, mambo huanza kila mmoja akijitenga katika kundi lake na kupambana kivyake dhidi ya kila mmoja atakayekwenda mbele yake.
Hapa hakuna mdogo tena, kila mmoja hupambana kupitia anachoona kitamuwezesha kupata sare au ushindi yaani pointi moja au tatu ni lazima na adui mkuu anakuwa ni kupoteza.
Angalia, vinara wa ligi hiyo kwa sasa, Yanga huenda ndio wenye hofu kubwa kuliko hata timu iliyo katika nafasi ya 15 na hii inatokana na kwamba baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza bila ya kufungwa hata mechi moja, viongozi wengi wakaamini ni wakati wa kutangaza ubingwa.
Kiuhalisia walitakiwa kuacha kikosi chao kicheze angalau mechi tano za mzunguko wa pili ili kujua mwendo wao halisi wa mzunguko huo maana mwendo wa mizunguko miwili huwa tofauti kutokana na hali halisi.Uchezaji wa kila timu katika mzunguko wa pili huwa una presha, nguvu na kujituma zaidi kwa kuwa kila mmoja anaanza kuhisi yuko hatarini na analazimika kupambana hasa ili kufikia malengo ya anachokihitaji.
Wakati fulani ilikuwa vigumu sana kuelezea kuwa Yanga bado inahitaji kujenga kikosi chake kwa kuwa si imara kama ambavyo uongozi na mashabiki wanaamini na hii ilitokana na ile hali ya “Unbeaten”, maana haijafungwa mzunguko mzima.
Ikaamsha matumaini makubwa yaliyopita uhalisia na kila aliyejaribu kusema lolote hasa kuhusu uhalisia au kukumbusha bado ligi ni ndefu na ugumu zaidi utakuwa katika mzunguko wa pili, tusubiri na kama Yanga itaanza na kufanya vizuri wakati huo, basi tutaona wameweza kufikia kiwango cha kusema wanaweza kuwa mabingwa, ulionekana umetumwa.
Sasa uhalisia unaanza kujionyesha, kwamba Yanga wanahitaji kuendelea kupambana lakini si kuamini kile wasichonacho mkononi. Sasa wamefikia mechi ya 22, yaani mechi tano baada ya kuingia mzunguko wa pili.Katika mechi hizo tano za mzunguko wa pili, Yanga wameshinda mechi moja, sare tatu, wamepoteza moja.
Hii maana yake iko hivi, ndani ya mechi hizo tano za mzunguko wa pili, pamoja na kupoteza, Yanga wamedondosha pointi tisa, maana yake wamekusanya pointi 6 katika mechi tano.
Kama wangeshinda zote wangestahili 15.Unaona wamekusanya sita na kudondosha tisa na ndio mechi tano za kwanza. Maana yake wana mechi 12 mkononi.
Jiulize, wataweza kusimama tena na kurudi katika mwendo wao? Maana kama Yanga wataendelea na mwendo huu ndani ya mechi nyingine tano, bila kupoteza muda, hakuna nafasi tena ya ubingwa.
Hii ni kwamba kikosi chao ni kizuri lakini hakijawa na ubora wa kusimama katika mwendo wa mzunguko wa pili ambao una nafasi kubwa kupima ubora wa kikosi ulichonacho.
Baada ya mzunguko wa kwanza, ukiingia wa pili na kufanikiwa kusimama vizuri, maana yake kikosi chako kina ubora wa kuvuka ugumu wa mzunguko wa pili.
Bahati moja wamepata Yanga, kikosi chao kimeyumba mwanzoni mwa mzunguko wa pili, wameona mapema. Wanachotakiwa ni kurekebisha baadhi ya mambo kama makosa waliyoyaona badala ya kutumia muda mwingi kusukuma lawama nje yao.
Wakati Yanga wamepata sare mfululizo, hawakutulia na kujiuliza kinachofanya chombo chao kuyumba. Moja kwa moja walikurupuka na kuanza kuwatupia watu lawama. Sasa uhalisia unaanza kuonekana, Yanga inacheza mechi tano ikiwa na ushindi mmoja, sare tatu na kupoteza moja, kweli huku ni kuonewa?
Najua, binadamu hatupendi kuelezwa ukweli sababu ya asili ya ukweli una maumivu. Lakini kumbuka, kama hutaki kuambiwa ukweli na wakweli, basi hali halisi itasema ukweli na utashindwa kuupinga.
Sasa ukweli unaendana na hali halisi na Yanga hawasemi tena wanaonewa kwa kuwa wanaona kinachotokea ni uhalisia.
Sasa swali, wanafanya nini kurekebisha ili waende mwendo sahihi?Kocha na benchi lake la ufundi wakutane, baada ya hapo wakae na wacheaji wao halafu wafanye kikao cha pamoja na uongozi na kamati za ufundi na lengo liwe kuangalia tatizo na si kulaumiana na kama hawataki haya, Yanga itaendelea kupoteza au kudondosha pointi na mwisho litakuwa ni suala la kutafuta mchawi ambaye hatapatikana.
MAKALA NA SALEH ALLY
Usimwamshe aliyelala, akiamka utalala wewe.
ReplyDeleteHao hwataki kusikia wala kuona Mpaka jahazi lizame kwasababu sikio la kufa halisikii dawa
ReplyDeleteNilishawahi sema kuwa yanga hawachezi vzr ila kinachowabeba ni hamasa inayowafanya wacheze kwa nguvu zao zote, nikasema hali hii itafika wkt watachoka lkn wakapinga. Sasa ndo wanayaona
ReplyDeleteKaze aneshaanza kukata pumzi. Wachezaji sio wana ya kiivyo tatizo liko kwenye ufundishaji
ReplyDelete*wabaya
ReplyDeletePenye kuonewa patasemwa, na pataonekana na pa udhaifu wao panaonekana, haina maana kuwa unatakiwa kuonewa kwa kuwa ni dhaifu hapana.
ReplyDeletekweri
DeleteHilo ndio tatizo la soka la kibongo kila kukicha lawama mm sioni tatizo kwa kocha ila shida iko kwa baadhi ya viongozi huwa wanataka kupiga pesa tuu na ndio hivyo soka la bongo halitoendelea
ReplyDeleteSaleh jembe leo umeichambua Yanga vizuri sana. Huu ndio ukweli hasa. Kocha alipaswa kuwaongoza viongozi ili kuelekeza nguvu kuiweka timu vizuri ili angalau wapate ubingwa mwaka huu. Ukarabati wa jengo na kikao na waandishi wa habari siyo kipaumbele sana kwa timu na washabiki kwa sasa ambayo haikupata ubingwa kwa miaka 3 mfululizo
ReplyDelete